Mipango yasukwa kuimaliza rushwa

DODOMA: Serikali imepanga kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa katika mwaka wa fedha 2026/27, ikiwemo kufanya utafiti wa kitaifa wa hali ya utawala na rushwa nchini (National Governance and Corruption Survey – NGACS).
Akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya wizara hiyo bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete amesema kuwa TAKUKURU pia itaendelea kuimarisha usimamizi wa matumizi ya fedha za umma katika miradi ya maendeleo ili kuhakikisha thamani halisi ya fedha inazingatiwa.
Alieleza kuwa taasisi hiyo itafanya uchunguzi wa majalada ya tuhuma za rushwa yanayoendelea pamoja na kushughulikia tuhuma mpya zitakazojitokeza, huku ikiendesha mashauri ya rushwa mahakamani kwa kibali cha Mkurugenzi wa Mashtaka.
Waziri Kikwete amebainisha kuwa TAKUKURU pia itakamilisha na kuanza kutumia mfumo wa takwimu na uchunguzi, sambamba na kufanya tafiti na uchambuzi wa mifumo ya utoaji huduma katika sekta za ajira, elimu, afya na ukusanyaji mapato ya serikali ili kubaini mianya ya rushwa na kupendekeza njia za kuiziba.
Hatua hizo zinatarajiwa kuongeza ufanisi katika vita dhidi ya rushwa na kuimarisha utawala bora nchini.



