KCMC yahimiza uchangiaji ujenzi kituo cha moyo

DAR ES SALAAM: UONGOZI wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) umeomba wananchi wa ndani na nje ya nchi kuendelea kuunga mkono juhudi za ujenzi wa kituo kikubwa cha matibabu ya magonjwa ya moyo.

Akizungumza katika hafla ya utiaji saini makubaliano ya uchangishaji fedha kati ya KCMC na kampuni ya Halotel, Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Profesa Gilead Masenga, amesema ushirikiano huo unalenga kuimarisha ukusanyaji wa rasilimali kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa kituo hicho, ambao umefikia asilimia 40.

Amesema kupitia makubaliano hayo, kampeni ya kitaifa ya uchangishaji fedha itaanzishwa ili kuhakikisha upatikanaji wa fedha za kukamilisha kituo cha kisasa cha magonjwa ya moyo na mishipa.

Profesa Masenga amebainisha kuwa magonjwa yasiyoambukiza yanachangia takribani asilimia 70 ya vifo duniani, huku magonjwa ya moyo na mishipa yakiongoza. Kutokana na hali hiyo, alisisitiza umuhimu wa kuwekeza katika miundombinu na huduma za kisasa za matibabu ya moyo nchini.

Kwa mujibu wake, hospitali hiyo inahitaji takribani Shilingi bilioni tatu kukamilisha ujenzi huo, baada ya wadau kutoka Marekani kuchangia sehemu kubwa ya gharama ya jumla inayokadiriwa kufikia Shilingi bilioni 50, ikijumuisha ujenzi na ununuzi wa vifaa tiba.

Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa HaloPesa, Magesa Wandwi, amesema kampuni hiyo imeguswa na jitihada za KCMC katika kushughulikia changamoto ya magonjwa ya moyo nchini.

Amesema kupitia huduma ya HaloPesa, wameandaa jukwaa rahisi na salama litakalowawezesha Watanzania kuchangia kwa urahisi zaidi, bila makato yoyote kwa watumiaji wa Halotel.

Wandwi alieleza kuwa wananchi wanaweza kuchangia kupitia namba maalum ya malipo (Lipa Namba) 23758475, kwa jina la “KCMC Moyo”, hatua inayolenga kuongeza ushiriki wa jamii katika kukamilisha mradi huo muhimu wa afya.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button