Ng’ongo yapata zahanati mpya

WANANCHI wa Kijiji cha Ng’ongo, Wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa, wameanza kunufaika na huduma za afya zilizo karibu na makazi yao baada ya kukamilika na kuzinduliwa rasmi kwa Zahanati ya Ng’ongo kwa gharama ya Sh milioni 265.
Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Ng’ongo, Dk Homera amesema kukamilika kwa zahanati hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Afya pamoja na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), inayolenga kuhakikisha huduma za msingi za afya zinawafikia wananchi katika maeneo wanayoishi.
Amesema Serikali imeendelea kuweka mkazo katika kuboresha sekta ya afya kwa kujenga na kuimarisha miundombinu ya kutolea huduma, hatua inayosaidia kupunguza changamoto ya wananchi kutembea umbali mrefu kufuata matibabu.
“Serikali itaendelea kuhakikisha huduma muhimu zinawafikia wananchi kwa wakati na kwa urahisi, hasa katika maeneo ya vijijini ambako wananchi wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya umbali wa vituo vya afya,” alisema.

Kwa upande wake, mkazi wa Kijiji cha Ng’ongo, Justin Kilatu, alisema uwepo wa zahanati hiyo umeondoa changamoto kubwa iliyokuwa ikiwasumbua wananchi ya kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma za afya. “Tulikuwa tunatembea umbali mrefu kupata matibabu, lakini sasa huduma zipo karibu nasi. Tunaishukuru Serikali kwa kutusikiliza na kutuletea huduma hii muhimu,” alisema Kilatu.
Naye mkazi wa kijiji hicho, Zena Amri, alisema kukamilika kwa Zahanati ya Ng’ongo ni ishara ya jitihada zinazoendelea za Serikali katika kuimarisha huduma za afya vijijini. Amesema uwepo wa kituo hicho utasaidia wananchi kupata huduma bora kwa wakati na kupunguza changamoto zilizokuwa zikijitokeza kutokana na umbali wa kufuata matibabu.
Tangu zahanati hiyo ianze kutoa huduma mwezi Novemba 2025, jumla ya wananchi 8,550 wamehudumiwa kupitia huduma mbalimbali za afya, hali inayoonyesha umuhimu wa uwekezaji huo katika kuboresha ustawi wa jamii. SOMA: Wananchi 16,000+ kunufaika na zahanati Mirerani



