Wananchi 16,000+ kunufaika na zahanati Mirerani

MANYARA: ZAIDI ya wananchi 16,000 wakiwemo wachimbaji wa madini na wadau mbalimbali wa shughuli za kiuchumi wanatarajiwa kunufaika na Zahanati Mpya inayojengwa katika eneo tengefu la Mgodi wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara.
Hayo yamebainishwa leo Juni 3, 2026 Katibu wa NEC, Itikadi Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Kenani Kihongosi alipotembelea na kukagua ujenzi wa Zahanati hiyo ambao ni sehemu ya uwajibikaji wa Jamii (CSR).
Akizungumza mara baada ya kukagua na kupokea taarifa ya mradi huo Kihongosi amepongeza kampuni ya Franon Mining kwa kuonesha mfano wa uzalendo kwa kutekeleza kwa vitendo dhana ya CSR.
Amesisitiza kuwa sheria na miongozo ya serikali inataka makampuni yote yanayofanya shughuli za uchimbaji kurejesha sehemu ya faida kwa jamii.

Amesema CSR si hisani bali ni wajibu wa kisheria na kijamii, akibainisha kuwa kampuni zinazoshindwa kufanya hivyo zinapaswa kuwajibishwa, kwani wananchi wanaoishi katika maeneo ya migodi wanastahili kunufaika moja kwa moja na rasilimali zinazozalishwa katika maeneo yao.
“Hawa wameonesha uzalendo, wameonesha utii kwa Serikali, wamejenga kituo cha afya, kampuni nyingine lazima zifanye kwa sababu zisipofanya, maana yake wanakiuka utaratibu wa serikali wakirudisha kwa jamii, kwa sababu kama wananchi wanaishi, lazima wapewe huduma,” amesema Kihongosi.
Akitoa taarifa ya ujenzi wa mradi huo Meneja wa Kampuni ya Franone Mining &Gems, Vitus Ndakize amesema mradi huo wenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 200 umetekelezwa kwa ufadhili wa kampuni hiyo pamoja na kutoa eneo la ujenzi.

Pia amesema lengo kuu la mradi huo ni kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa wadau wa sekta ya madini wakiwemo wachimbaji, wafanyabiashara na watoa huduma nyine katika eneo hilo.
Amesema zahanati hiyo inajumuisha miundombinu muhimu ikiwemo chumba cha mapokezi, cha daktari,sindano, cha kufunga vidonda, maabara, ofisi ya utawalana vyumba viwili vya wagonjwa kwa ajili ya uangalizi.
Pia ina chumba cha chanjo, wajawazito, cha kutolea dawa, na kuhifadhi dawa na stoo maalumu ya kuhifadhia mitungi ya oksijeni, yote yakilenga kuboresha utoaji wa huduma bora za afya kwa wananchi.



