Madini ya bil 3/- yanaswa yakitoroshwa

DODOMA: Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amesema kuwa katika kipindi cha Julai 2025 hadi Machi 2026, wizara yake kwa kushirikiana na mamlaka nyingine za Serikali imefanikiwa kukamata madini ya aina mbalimbali yenye thamani ya shilingi bilioni 3.31 katika matukio 55 yaliyotokea kwenye baadhi ya mikoa ya kimadini nchini.
Akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Madini kwa mwaka wa fedha 2026/2027 bungeni jijini Dodoma, Waziri Mavunde amesema madini yote yaliyokamatwa yalitaifishwa na Serikali, huku watuhumiwa wakichukuliwa hatua za kisheria kwa kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Waziri Mavunde amesisitiza kuwa hatua hizo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kudhibiti vitendo vya utoroshaji wa madini vinavyofanywa na baadhi ya wachimbaji na wafanyabiashara wasio waaminifu.
Aidha, ametoa rai kwa wachimbaji na wafanyabiashara wa madini nchini kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zote zinazosimamia biashara ya madini ili kuepuka hasara na migogoro na vyombo vya dola.
Katika hatua nyingine, Waziri Mavunde ameeleza kuwa mapato ya fedha za kigeni yatokanayo na mauzo ya madini nje ya nchi yameendelea kuimarika mwaka hadi mwaka.
Amebainisha kuwa mwaka 2025, thamani ya mauzo ya madini nje ya nchi ilifikia dola za Marekani milioni 5,401.9, hali inayoonesha mchango mkubwa wa sekta ya madini katika kukuza uchumi wa taifa.



