Tanzania kinara wa graphite Afrika

MJIOLOJIA kutoka Ofisi ya Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Njombe, Abbas Mruma, amesema Tanzania inaendelea kujijengea nafasi muhimu duniani kutokana na kuwa na hifadhi kubwa ya madini ya kimkakati, yakiwemo graphite, lithium na rare earth elements, yanayotumika katika teknolojia za kisasa na nishati safi.

Mruma amesema hayo alipokuwa akitoa maelezo kwa Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dk. Richard Stanslaus Muyungi, aliyetembelea banda la Tume ya Madini kwenye Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba). SOMA: Mavunde: Tanzania kuwa kitovu cha uchakataji madini Afrika

Amesema mahitaji ya madini ya lithium yanaongezeka duniani kutokana na matumizi yake katika utengenezaji wa betri za magari ya umeme, simu za mkononi, kompyuta mpakato na vifaa vingine vya kielektroniki. Aibainisha kuwa nchini Tanzania madini hayo yanapatikana zaidi katika maeneo ya Dodoma na Ikungi mkoani Singida.

Kuhusu graphite, Mruma amesema Tanzania inaongoza Afrika kwa kuwa na hifadhi kubwa ya madini hayo, ambayo ni malighafi muhimu katika utengenezaji wa betri za magari ya umeme na bidhaa nyingine za viwandani. Amesema Tanzania ina hifadhi kubwa ya madini ya rare earth elements katika Ukanda wa Afrika Mashariki, yanayopatikana Ngualla mkoani Songwe na Wigu mkoani Morogoro.

Baada ya kupokea maelezo hayo, Dk. Muyungi aliipongeza Tume ya Madini kwa kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu rasilimali za madini na fursa zilizopo katika sekta hiyo. Amesema elimu hiyo inaongeza uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa rasilimali za madini, fursa za uwekezaji na mchango wa sekta ya madini katika kukuza uchumi na maendeleo endelevu ya taifa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button