Serikali yatenga Sh bilioni 200 kwa wananchi

DODOMA: Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 200 kwa ajili ya kuwezesha shughuli mbalimbali za kiuchumi nchini kote, ikiwemo sekta za kilimo, ufugaji wa mifugo pamoja na uvuvi wa samaki, Ili kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia fursa mbalimbali za kifedha zinazotolewa na wizara pamoja na mifuko ya maendeleo iliyoanzishwa na Serikali.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu , Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI) Dk Festo Dugange alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Kagera, Devotha Daniel leo Aprili 28, 2026, Bungeni jijini Dodoma, aliyetaka kufahamu kama Serikali ipo tayari kutenga dirisha maalum la mikopo kwa sekta za kipaumbele za kilimo cha kahawa, ufugaji na biashara ndogondogo mkoani Kagera.

Dk Dugange amebainisha kuwa fedha hizo ni sehemu ya mkakati mpana wa Serikali wa kuhakikisha kila Mtanzania ananufaika na rasilimali za nchi na kwamba Serikali imejipanga kutoa elimu na hamasa kwa jamii ili makundi yaliyokusudiwa yaweze kuchangamkia fursa hizo adhimu ambayo imekuja wakati kukiwa na hitaji kubwa la mitaji miongoni mwa wajasiriamali wadogo na wa kati ili kukuza mnyororo wa thamani katika mazao ya biashara.
“Kwa sasa Wizara ya Mifugo na Uvuvi imetoa matangazo ya kutoa mikopo ya shilingi bilioni 200 ambazo ni ahadi ya Dk Samia Suluhu Hassan ya kuwezesha wananchi kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kiuchumi zikiwemo kilimo, ufugaji wa mifugo na samaki,” amesema Dk Dugange.
Mbali na fedha hizo za ahadi ya Rais, Serikali imesisitiza kuwa bado kuna madirisha mengine ya mikopo ikiwemo ile ya asilimia 10 inayotokana na mapato ya ndani ya halmashauri. Katika Mkoa wa Kagera pekee, Serikali imeshatoa shilingi milioni 742.67 kupitia mfumo huo wa asilimia 10 kwa mwaka wa fedha 2024/25. Hii imedhihirisha azma ya dhati ya Serikali katika kuhakikisha kuwa mzunguko wa fedha unafika hadi kwa mwananchi wa hali ya chini.

Amesema Serikali imewahakikishia Watanzania kuwa mikopo hiyo haina ukiritimba na inatolewa kwa taratibu rafiki ili kila mwenye sifa aweze kunufaika na amewataka wakulima na wafanyabiashara kote nchini kutumia fursa hizo kujiimarisha kiuchumi na kurejesha fedha hizo kwa wakati ili ziweze kuwanufaisha wengine. Hatua hii imetajwa kuwa ni nguzo muhimu katika kuelekea uchumi wa kati wenye tija na ushindani katika soko la ndani na nje ya nchi.



