Wadakwa kwa kupunguza vipimo kwenye vifungashio

GEITAL WAKALA wa Vipimo Tanzania (WMA) Mkoa wa Geita imebaini dosari na udanganyifu wa vipimo katika baadhi ya bidhaa zenye vifungashio kwenye maduka ya jumla na rejareja.

Meneja wa WMA mkoa wa Geita, Eva Ikula ametoa taarifa hiyo katika mahojiano maalumu na HabariLEO na kueleza kuwa changamoto hiyo imebainika katika ukaguzi wa kushtukiza uliofanyika hivi karibuni.

Eva amesema uchunguzi umebaini kuwa bidhaa nyingi zenye changamoto ya vipimo sahihi ni bidhaa za nafaka ikiwemo unga wa ngano na sembe ambapo wafanyabiashara hupunguza.

Amesema katika msako uliofanyika mwezi Machi 2026 wafanyabiashara watano walitiwa mbaroni kwa kupunguza kiwango cha bidhaa za nafaka pamoja na sukari na tayari walichukuliwa hatua.

“Ofisi yetu imeweza kubaini kwamba ufungashaji wa bidhaa za unga una changamoto ya kufungasha bidhaa ambazo zipo chini ya uzito uliopaswa kuwa umefungashwa kwenye bidhaa.

“Wale wote ambao walibainika na kukutwa na makosa ya ufungashaji pungufu ya kile kilichoidhinishwa waliweza kuchukuliwa hatua za kulipa faini”, amesema Eva.

Amesema ufuatiliaji unaendelea kuwachukulia hatua wote wanaotenda kosa la ufungashaji pungufu kwani ni kinyume na sheria ya vipimo sura namba 340.

Amesema mfanyabiashara anayebainika kuchezea kwa makusudi mizani ama kipimo cha bidhaa aliyoifungasha adhabu yake ni kiasi cha sh laki moja mpaka milioni 20 kwa kosa la kwanza.

Eva amesema kwa mjibu wa sheria ya vipimo mfanyabiashara anapothibitika kutenda kosa hilo kwa mara ya pili adhabu yake ni kiasi cha sh laki tano hadi milioni 50.

Habari Zifananazo

One Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button