Wakili aeleza uhalali wa mwekezaji Shamba Na 1135 Magunga Iringa

IRINGA: Maelezo ya kina yaliyotolewa na wakili wa kampuni ya Iringa Food and Beverages Ltd (IFB), Innocent Boniface yametoa mwelekeo katika mgogoro wa umiliki wa Shamba Na. 1135 lililopo Kijiji cha Magunga, wilayani Iringa baada ya kufafanua mnyororo mzima wa umiliki unaoonyesha kuwa eneo hilo linamilikiwa kihalali na mwekezaji.
Kupitia wakili huyo, upande wa mwekezaji umeweka wazi nyaraka, historia ya umiliki na taratibu zote za kisheria zilizofuatwa hadi kupatikana kwa hati rasmi ya eneo hilo, hatua ambayo imeelezwa kuwa inaweza kumaliza sintofahamu iliyodumu kwa muda.
Kwa mujibu wa wakili Boniface, eneo hilo halikuchukuliwa kwa mabavu wala kwa njia ya kificho, bali lilinunuliwa kwa utaratibu halali kutoka kwa wamiliki waliokuwa na haki za kisheria juu ya mashamba yao.
Alisema mmiliki wa kwanza alikuwa Joshua Nyangoya, aliyekuwa na Shamba Na. 102 lenye takribani ekari 200, huku mmiliki wa pili akiwa Godliven Joshua Mandari, aliyekuwa na Shamba Na. 83 lenye ukubwa unaokadiriwa kufikia ekari 200.
Kwa mujibu wa maelezo hayo, mashamba yote mawili yalikuwa tayari yamepimwa, kusajiliwa na kupewa hati miliki na mamlaka husika kwa mujibu wa sheria za ardhi zilizokuwa zinatumika wakati huo.
Wakili huyo alifafanua kuwa hati ya Joshua Nyangoya ilitolewa Machi 10, 1989, huku hati ya Godliven Mandari ilitolewa Septemba 16, 1988, jambo linalodhihirisha kuwa maeneo hayo yalikuwa katika mfumo rasmi wa umiliki unaotambuliwa na serikali.
Baada ya ununuzi huo, mwekezaji alifuata taratibu zote zinazotakiwa kisheria ikiwemo uhamisho wa miliki, ulipaji wa kodi, ada za serikali na uhakiki wa nyaraka kabla ya umiliki kuhamishiwa rasmi kwa familia ya Thakore.
Familia hiyo inayoundwa na Ismail Thakore, Suhel Thakore na Isihaka Thakore, ndiyo inayotambulika sasa kama mmiliki halali wa eneo hilo kwa mujibu wa hati ya miaka 99 iliyotolewa tarehe 20 Januari 2023.
Boniface alisema hatua hiyo haikutokea kwa bahati mbaya, bali ilitokana na uchunguzi wa kina uliofanywa na taasisi za serikali zinazoshughulikia ardhi, zilizopitia historia ya eneo, nyaraka za awali na wajibu wote wa kisheria kabla ya kutoa hati mpya.
“Serikali haiwezi kutoa hati bila kujiridhisha kwanza. Hii ni uthibitisho wa wazi kuwa mteja wetu ni mmiliki halali,” alisema wakili huyo.
Katika ufafanuzi wake, Boniface alieleza kuwa mgogoro katika shamba hilo uliibuka baada ya baadhi ya watu kuuza maeneo yaliyopo ndani ya shamba hilo kwa wananchi bila kufuata taratibu za sheria na bila kuhakiki umiliki halali wa ardhi husika.
Alisema mauzo hayo ndiyo yaliyozalisha mkanganyiko uliosababisha baadhi ya wananchi kuamini kuwa walinunua maeneo halali, wakati ukweli ni kuwa ardhi hiyo tayari ilikuwa na mmiliki mwenye hati.
Akizungumzia madai ya kihistoria ya baadhi ya wananchi, wakili huyo alisema ni kweli baadhi yao waliwahi kuishi eneo hilo kabla ya Operesheni Vijiji ya mwaka 1978, lakini baadaye walihamishwa na serikali chini ya sera za upangaji wa makazi na matumizi ya ardhi.
Alisisitiza kuwa kwa mujibu wa sheria, historia ya makazi ya zamani haiwezi kufuta hati miliki halali iliyotolewa na mamlaka bila kufuata utaratibu wa mahakama au chombo chenye mamlaka.
Boniface aliongeza kuwa mwekezaji huyo ameendelea kuwa mvumilivu huku akiheshimu sheria za nchi, akiamini kuwa uwekezaji wa halali unapaswa kulindwa kwa manufaa ya maendeleo, ajira na mapato ya serikali.
“Wawekezaji wanaofuata sheria wanahitaji ulinzi wa uhakika. Ndiyo njia ya kujenga uchumi imara,” alisema.
Kutokana na maelezo hayo ya kisheria, wachambuzi wa masuala ya ardhi wanaona kuwa mgogoro huo sasa umeanza kupata mwanga, huku nyaraka zilizowekwa wazi zikionyesha kuwa haki ya umiliki ipo upande wa mwekezaji.
Wakati mamlaka husika zikiendelea kushughulikia suala hilo, upande wa mwekezaji umeeleza kuwa una imani kuwa ukweli uliowasilishwa, pamoja na nguvu ya hati halali, vitasaidia kumaliza kabisa mgogoro huo kwa njia ya sheria.



