REA yatekeleza mpango wa majiko banifu Kagera vijijini

BUKOBA: Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umeanza utekelezaji wa mpango wa kusambaza majiko banifu 200,000 nchini kwa lengo la kupunguza matumizi ya kuni na mkaa, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa taifa wa matumizi ya nishati safi unaolenga kufikia asilimia 80 ya wananchi waishio vijijini ifikapo mwaka 2034.

Kupitia mpango huo, REA imemtambulisha msambazaji wa majiko hayo kutoka kampuni ya BURN MANUFACTURING, ambaye atasambaza majiko katika mikoa minne nchini. Katika mkoa wa Kagera, jumla ya majiko banifu 12,000 yatagawiwa kwa wananchi wa vijijini.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mwandishi Mwandamizi kutoka REA, Deusdedith Malulu, alisema wakala huo unaendelea kubuni teknolojia rafiki za nishati ya kupikia ili kusaidia uhifadhi wa mazingira na kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanatumia nishati safi.

Alisema serikali imegharimia asilimia 80 ya gharama ya jiko hilo, ambapo mwananchi aliyetakiwa kulinunua kwa Shilingi 75,000, sasa atalipata kwa mchango wa Shilingi 12,500 pekee.

“Kwa mfano majiko yaliyokuja Kagera mradi wake ulikuwa wa shilingi milioni 700, lakini serikali imetoa shilingi milioni 600 na wananchi watachangia shilingi milioni 100 tu kama watachukua majiko yote. Hii ni nia ya dhati ya serikali kuhakikisha wananchi wanapata teknolojia za kupikia kwa gharama nafuu huku mazingira yakilindwa,” alisema Malulu.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera, Stephen Ndaki, alisema hatua hiyo ni muhimu kwa kuwa inawafikia wananchi wa vijijini hata wale wanaotumia kuni na mkaa, akisisitiza mgawanyo sawa katika halmashauri zote saba za mkoa huo.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera ameipongeza REA kwa kutekeleza maelekezo ya Rais, huku akisisitiza kuwa usambazaji wa majiko hayo uendane sambamba na utoaji wa elimu ya utunzaji wa mazingira.

Kwa upande wake, msambazaji wa majiko hayo kutoka BURN MANUFACTURING, John Mtui, alisema mwananchi atakayepata jiko hilo kwa ruzuku anatakiwa kuwa na kitambulisho cha Taifa na kuchangia Shilingi 12,500.

Alisema majiko hayo yana sifa za kutumia mkaa kidogo, kutotoa moshi, kupika kwa haraka na kuwa na uimara wa muda mrefu.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button