Dar kujengwa kituo maalumu kuimarisha uwezo wa walimu

DAR ES SALAAM: HALMASHAURI ya Jiji la Dar es Salaam imetenga Sh bilioni 432 kwa ajili ya ujenzi wa kituo maalumu cha umahiri kitakacholenga kuinua ubora wa elimu cha Edward Jonas Mpogolo Center for Excellence Capacity Building, ili kuongeza uwezo wa walimu na kuboresha usimamizi wa mitihani ya ndani.

Hatua hiyo imetangazwa katika hafla ya kutangaza matokeo ya mitihani ya ndani ya shule za sekondari za jiji hilo na kutoa tuzo kwa shule zilizofanya vizuri kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza, cha pili, cha tatu na cha sita.

Shule zilizofanya vibaya zilikabidhiwa vinyago maalumu vya mpingo kama sehemu ya kuhamasisha uwajibikaji na kuongeza juhudi katika kuboresha matokeo.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, alisema uwekezaji huo ni sehemu ya mkakati wa kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 pamoja na maono ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan ya kuimarisha sekta ya elimu nchini.

Alisema lengo ni kuboresha miundombinu ya elimu na kuhakikisha wanafunzi wanahitimu wakiwa na maarifa na ujuzi unaokidhi mahitaji ya maendeleo ya taifa.

Mpogolo alisema Jiji la Dar es Salaam linaendelea kujenga shule za sekondari za ghorofa zenye vifaa vya kisasa, kuongeza upatikanaji wa vitabu, kuimarisha nidhamu na uwajibikaji, kutumia teknolojia katika ufundishaji na kujifunza, pamoja na kutekeleza mkakati wa kuondoa daraja sifuri na daraja la nne katika matokeo ya mitihani.

Alipongeza uamuzi wa halmashauri hiyo wa kujenga kituo hicho na kukipa jina lake, akisema kitakuwa chachu ya kuongeza ufaulu wa wanafunzi, kuimarisha uwezo wa walimu na kuboresha tathmini ya elimu.

Awali, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Elihuruma Mabelya, alisema kituo hicho kitakuwa kitovu cha mafunzo na tathmini za elimu, huku kikisaidia kuimarisha mfumo wa mitihani ya ndani.

“Kituo hiki kitakapokamilika kitasaidia kuboresha usimamizi wa mitihani, kuongeza umahiri wa walimu na kujenga mfumo madhubuti wa mitihani ya ndani unaofanana na ule wa Baraza la Mitihani la Taifa,” alisema.

Mabelya alisema halmashauri hiyo pia inaendelea na maandalizi ya kupokea wanafunzi 89,782 wa mfumo wa double cohort mwaka 2028, jambo linalohitaji uwekezaji mkubwa katika miundombinu na kuboresha ubora wa elimu.

Alisema kwa sasa kiwango cha ubora wa ufaulu wa jiji hilo ni asilimia 35, huku lengo likiwa kufikia asilimia 50 na kuingia miongoni mwa halmashauri tatu bora nchini katika matokeo ya mitihani ya taifa.

Kwa upande wake, Ofisa Elimu Sekondari wa Jiji la Dar es Salaam, Mussa Ally alisema utoaji wa tuzo hizo umetokana na tathmini ya matokeo ya mitihani ya ndani iliyoratibiwa na kamati maalumu, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuongeza ufaulu wa wanafunzi katika mitihani ya taifa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button