Mwang’onda aridhishwa mradi wa madarasa Mtwara Vijijini

MTWARA: KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2026, Wazo Mwang’onda ameridhishwa na mradi wa ujenzi wa vyumba vya viwili vya madarasa katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara Vijijini mkoani Mtwara uliyogharimu Sh milioni 49.5.
Mwenge wa Uhuru umepokelewa jana katika kijiji cha maili kumi kilichopo kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara mkoani humo ukitokea Manispaa ya Mtwara Mikindani.
Mwenge huo ukiwa katika halmashauri hiyo utapitia miradi mbalimbali ya maendeleo 5 yenye thamani ya zaidi Sh milioni 600 ikiwemo huo wa madarasa.

Pia upandaji wa miti katika mradi wa mazingira, uzinduzi wa klabu ya upingaji wa madawa ya kulevya na mingine huku ukikimbizwa umbali wa kilomita 72.
Aidha, katika miradi hiyo ikiwemo kuweka mawe ya msingi miradi miwili, mradi mmoja kufungua, mradi mmoja kuzindua pamoja na mradi mmoja kuona na kukagua.
Akizungumza leo Mei 4, 2026 alipokuwa akiweka jiwe la msingi mradi huo wa madarasa, kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa amesema mradi huo unaendelea vizuri na umefikia hatua ya umaliziaji.

“Tuwapongeze sana viongozi wa halmashauri hii ya Mtwara DC kwa usimamizi mzuri wa miradi, tunaipongeza sana serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuandaa madarasa haya”amesema Wazo
Pia amewaomba viongozi wa halmashauri hiyo kuendelea na maandalizi hayo kwa kujenga madarasa mengine na kutafuta madawati ili watoto waje wasome katika mazingira yaliyo bora.
Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Abdallah Mwaipaya amesema ujenzi wa mradi huo wa madarasa ni kwa ajili ya kuweka utaratibu mzuri wa kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza Januari 2028.



