Emanuela Mtatifikolo: “Narudi Nyumbani” kuitumikia Isimani

IRINGA: Mgombea ubunge wa Jimbo la Isimani kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Emmanuela Kaganda Mtatifikolo, ameanza rasmi safari yake ya kuwania nafasi hiyo kwa kauli yenye uzito wa kihisia na kisiasa “Narudi nyumbani.”
Kauli hiyo haikuwa ya kawaida. Ilibeba historia, uhalisia na dhamira ya kiongozi aliyelelewa na kukulia ndani ya ardhi ya Isimani.
Amezaliwa Desemba 25, 1978 na kukulia na kusoma shule ya msingi Idodi katika kijiji cha Idodi jimboni Isimani, ni mzawa halisi wa jimbo hilo, anayezifahamu kwa karibu changamoto na mafanikio ya wananchi wa eneo hilo.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa rasmi fomu za kugombea ubunge na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) katika ofisi za Ihemi, Emmanuela alisema kurejea kwake Isimani si bahati mbaya bali ni mwitikio wa dhamira ya ndani ya kulitumikia jimbo lake.
“Nimetokea kazini, nakuja kazini. Nimerudi nyumbani kuwatumikia watu wangu,” alisema kwa msisitizo.
Zoezi hilo lilisimamiwa na Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Isimani, Caroline Ang’weni Otieno, na kushuhudiwa na viongozi mbalimbali wa chama na serikali, akiwemo Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Iringa Vijijini, Costantino Kihwele, pamoja na mamia ya wanachama waliojitokeza kuonesha mshikamano.

Akizungumza na viongozi wa kata zote 13 za jimbo hilo mara baada ya kuchukua fomu hizo, Emmanuela alieleza kuwa anaijua vizuri Isimani akieleza kuwa uzoefu wake wa maisha ya jimbo hilo unampa uelewa wa moja kwa moja wa mahitaji ya wananchi.
“Nimelelewa hapa, nimesoma hapa, naijua Isimani. Nafahamu mafanikio yaliyopatikana na changamoto zilizopo, na nipo tayari kuzifanyia kazi,” alisema.
Kwa mujibu wa wasifu wake, Emmanuela ni kiongozi mwenye uzoefu mpana katika utumishi wa umma na sekta binafsi. Kwa sasa anahudumu kama Mkuu wa Wilaya ya Babati tangu mwaka 2024, baada ya kuwa Mkuu wa Wilaya ya Arumeru kuanzia 2023 hadi 2024.
Pia aliwahi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Jitegemee Holdings Co. Ltd, akisimamia miradi mbalimbali ya maendeleo.
Aidha, amewahi kufanya kazi katika taasisi za kitaifa na kimataifa ikiwemo Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere (Kibaha), Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA), na taasisi ya UEM, ambako aliratibu miradi katika nchi mbalimbali za Afrika na Asia.

Kitaaluma, Emmanuela ana Shahada ya Uzamili ya Afya ya Jamii (MPH) kutoka Chuo Kikuu cha Jiji la New York (CUNY), pamoja na Shahada ya Sanaa katika Mawasiliano ya Umma kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT), Mwanza mchanganyiko unaomjengea uwezo wa kusimamia maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa ufanisi.
Akizungumzia dira yake kwa Isimani, Emmanuela aliahidi kuendeleza misingi ya maendeleo iliyoachwa na aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, marehemu William Vangimembe Lukuvi, akimtaja kama kiongozi aliyeitumikia vyema jamii.
Alieleza kuwa miongoni mwa vipaumbele vyake atakapochaguliwa kuwa ni pamoja na kushirikishana na wananchi, serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo kuboresha sekta mbalimbali zinazohudumia jamii ikiwa ni pamoja na afya, elimu, maji, pamoja na kusukuma mbele maendeleo ya miundombinu ya barabara, umeme, kilimo, biashara na nyinginezo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Iringa Vijijini, Costantino Kihwele, aliwataka wanachama wa chama hicho kushikamana na kuhakikisha ushindi katika uchaguzi mdogo unaotarajiwa kufanyika Juni Mosi mwaka huu.
“Tushirikiane wana Kalenga na Isimani. Wilaya ni moja, nguvu iwe moja. Tutafanya kampeni za hoja na ushahidi wa kazi zilizofanyika,” alisema Kihwele.
Katika hotuba yake, Emmanuela aliwataka pia wananchi kuacha tofauti za kisiasa baada ya mchakato wa kura za maoni na kuungana kwa lengo la maendeleo.
“Sio kosa kuwa na upande wakati wa kura za maoni, lakini sasa tuna mgombea mmoja. Tuungane tusonge mbele,” alisisitiza.
Aliwahimiza pia wagombea wenzake waliopita katika mchakato wa uteuzi kushirikiana naye, akiahidi kupokea mawazo yao na kuyatumia katika kulijenga jimbo hilo.
Kwa hisia za kipekee, Emmanuela alikumbuka namna alivyoguswa alipokuwa akirejea Isimani, akisikiliza wimbo wa “Narudi Nyumbani” wa Remmy Ongala, akisema ulimkumbusha safari yake na wajibu alionao kwa watu wake.
Alimalizia kwa ahadi nzito:
“Sitawaangusha. Nitawatumikia kwa uaminifu, weledi na nitasikiliza ushauri wenu. Huu ni wakati wa kufanya kazi, si wa maneno.”



