Amlilia spika, mbunge amlipe Sh milioni 11 anazodai

IRINGA: Mfanyabiashara wa vifaa vya umeme wa mjini Njombe, Erick Sambala, ameibuka hadharani akiomba msaada wa Spika wa Bunge, Mussa Azzan Zungu, kufuatia kile anachodai ni kucheleweshwa kwa malipo ya deni analomdai Mbunge wa Viti Maalum (Chaumma), Siglada Mligo, kwa miaka miwili sasa.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Iringa, Sambala alisema kuwa Machi 6, 2024 aliingia mkataba wa kibiashara na mbunge huyo uliohusisha mkopo wa vifaa vya muziki vyenye thamani ya Sh Milioni 18.5 kwa makubaliano ya kulipwa ndani ya miezi mitatu.

Hata hivyo, alisema makubaliano hayo hayakuheshimiwa, kwani hadi sasa amelipwa Sh Milioni 8.5 .

Alisema kiasi cha zaidi ya Sh milioni 11 pamoja na fidia ambayo hakuitaja inayohusisha kucheleweshwa kwa malipo na gharama zinginezo kimeendelea kubaki bila kulipwa.

Kutokana na hali hiyo, Sambala alisema alilazimika kuchukua hatua za kisheria Januari 2025 kwa kufungua kesi katika Mahakama ya Mwanzo Njombe, ambapo alishinda.

Hukumu ya kesi hiyo ya madai namba 7 ya mwaka 2025 ilitolewa Machi 27, 2025, ikimtaka mdaiwa kulipa fedha hizo.

Alisema upande wa mdaiwa ulikata rufaa katika Mahakama ya Wilaya Njombe, lakini rufaa hiyo ilitupiliwa mbali na Mahakama hiyo chini ya Hakimu Mkazi James Muhoni, ambaye aliidhinisha uamuzi wa mahakama ya mwanzo na kumthibitishia Sambala ushindi wa madai yake.

Pamoja na ushindi huo katika ngazi zote mbili za mahakama, Sambala anadai bado hajalipwa fedha zake, hali ambayo amesema imeathiri kwa kiasi kikubwa biashara yake.

“Fedha hii ni sehemu ya mtaji wangu. Kwa miaka miwili sasa imekwama, hali iliyosababisha kuyumba kwa biashara yangu. Kama fedha hiyo ingekuwa kwenye mzunguko, hali yangu kiuchumi ingekuwa tofauti kabisa,” alisema Sambala.

Alieleza kuwa mbali na hasara ya mtaji, amelazimika pia kutumia gharama kubwa kuendesha kesi hiyo, zikiwemo gharama za usafiri, ambazo sasa anapanga kuzidai mahakamani.

Sambala aliongeza kuwa kinachomuumiza zaidi ni kuona mtu aliyepewa dhamana ya kuwatetea wananchi anashindwa kuheshimu haki za msingi za mwananchi wa kawaida.

“Ni jambo la kusikitisha kuona kiongozi wa kisiasa anashindwa kutekeleza maamuzi halali ya mahakama. Namuomba Spika aingilie kati na aliangalie suala hili ili nipate haki yangu,” alisisitiza.

Mfanyabiashara huyo amesema amelazimika kuamua kupaza sauti kupitia vyombo vya habari ili kufikisha kilio chake kwa mamlaka husika na umma kwa ujumla kutokana na kile alichokiita ukosefu wa utekelezaji wa hukumu.

“Naomba mamlaka za juu, hususani ofisi ya Spika, kuingilia kati ili kuhakikisha narejeshewa fedha zangu. Kurejeshwa kwa fedha hizo kutaniwezesha kuboresha biashara na kuchangia maendeleo ya familia yangu pamoja na uchumi wa taifa,” alisema.

Juhudi zilifanyika kumpata Singlada Mligo kujibu kwanini hadi sasa hajalipa kiasi hicho cha fedha.

“Si ndiyo kazi yenu? Ameshatoa taarifa kwa waandishi wa habari… eeh, rusheni,” kabla ya kukata simu ghafla.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button