DC Kwimba asisitiza usimamizi wa karibu wa miradi

MWANZA: MKUU wa Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza, Ng’wilabuzu Lúdigija, amesistiza umuhimu wa kusimamia kwa ukaribu utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuhakikisha miradi yote inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali inakamilika kwa wakati uliopangwa.

Ludigija alisema hayo jana wakati wa kikao cha baraza la madiwani liliofanyika katika ukumbi wa Philip Mangula wilayani Kwimba mkoani Mwanza.

Aliwataka madiwani kushirikiana na watendaji wa kata pamoja na wananchi katika kufuatilia hatua zote za utekelezaji wa miradi hiyo ili kuhakikisha thamani ya fedha inaonekana kupitia huduma bora kwa wananchi.

“Madiwani hakikisheni mnasimamia miradi yote ya maendeleo katika maeneo yenu. Wananchi wanahitaji kuona matokeo ya fedha zinazokusanywa,” alisema.

Aidha, aliwataka watendaji wa kata kuongeza uwajibikaji na kufanya ufuatiliaji wa karibu wa miradi inayotekelezwa katika maeneo yao ili kuondoa changamoto za ucheleweshaji wa miradi.

Vile vile, amewapongeza viongozi, watendaji pamoja na madiwani wa Halmashauri kwa juhudi kubwa walizoonesha katika ukusanyaji wa mapato ya ndani, hali iliyowezesha halmashauri kuvuka malengo yaliyowekwa kwa kipindi husika.

Alisema mafanikio hayo yanaonesha namna ushirikiano uliopo kati ya viongozi na watendaji unavyoendelea kuleta matokeo chanya katika maendeleo ya Wilaya ya Kwimba.

Alisema mapato hayo ni msingi muhimu wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayolenga kuboresha huduma za kijamii kwa wananchi, ikiwemo elimu, afya, maji na miundombinu.

“Tunapaswa kuendelea kushirikiana ili kuongeza mapato zaidi kwa manufaa ya wananchi wetu. Mafanikio haya yanaonesha kuwa tukisimamia vizuri rasilimali zilizopo tunaweza kufikia maendeleo makubwa,” alisema Lúdigija.

Aliwakumbusha wataalamu wa ujenzi kufanya kazi kwa uadilifu na kuacha tabia ya kuongeza gharama za vifaa vya ujenzi bila sababu za msingi jambo ambalo limekuwa likisababisha baadhi ya miradi kushindwa kukamilika kwa wakati.

Alisema serikali haitavumilia uzembe wowote utakaosababisha miradi kuchelewa au kutekelezwa chini ya kiwango kinachotakiwa.

“Baadhi ya wananchi wamekuwa wakinipigia simu wakilalamikia ucheleweshaji wa miradi katika maeneo yao. Nataka iwe wazi kwamba mradi wowote ambao hautakamilika kwa wakati, wahusika watawajibishwa,” alisisitiza.

Akichangia katika kikao hicho, Diwani wa Kata ya Mhande, Ndege Deus, alisema madiwani wa Wilaya ya Kwimba wamejipanga kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na maendeleo yanayokusudiwa yanafikiwa.

Alisema usimamizi madhubuti wa miradi pamoja na ushirikiano kati ya viongozi na wananchi ni msingi muhimu wa kuharakisha maendeleo katika wilaya hiyo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button