‘Elimu usalama barabarani itaokoa maisha ya wananchi’

DAR ES SALAAM: MBUNGE wa Jimbo la Mbagala, Burchard Kakulu amesema elimu ya usalama barabarani inayotolewa kwa waendesha bodaboda ni muhimu katika kuokoa maisha ya wananchi pamoja na kuchochea maendeleo ya taifa.

Kakulu amesema hayo kwenye uzinduzi wa mwendelezo wa kampeni ya Usalama Daima chini ya Azam Mediai iliyofanyika katika viwanja vya Zakhiem Mbagala, Temeke Dar es Salaam, kampeni inayolenga kufika mitaani, wilayani, mikoani na nchi nzima kuhamasisha usalama barabarani kwa madereva wa bodaboda na watumiaji wa barabara kwa ujumla.

“Katika maisha hata ungekuwa na maono mazuri, ndoto kubwa na mawazo mazuri kiasi gani, kama hauko salama kiafya havina maana yoyote.

Elimu wanayopewa vijana hawa maofisa usafirishaji sio tu muhimu kwao bali hata sisi watumia huduma,” amesema Kakulu.

Kwa upande wake, Meneja wa Mawasiliano na Mahusiano wa Azam Media⁠, Christina Korosso amesema kampeni hiyo inalenga kuhakikisha elimu ya usalama barabarani inawafikia waendesha bodaboda nchini kote.

“Tulianza na Kimara, tumekuja Mbagala na baadaye tutaenda Ilala tukiwa tumeshirikiana na Jeshi la Polisi, LATRA, Damu Salama, Car and Gear na TVS tunaamini mtu anapojifunza jambo mara kwa mara anakuja kulizoea,” amesema Korosso.

“Hawa maofisa usafirishaji ndio wanaotubeba sisi na watoto wetu. Wakifuata mafunzo haya ya kuvaa kofia ngumu na vifaa vya kujikinga watajilinda wao pamoja na abiria,” amesema.

Diwani wa Kata ya Mbagala Kuu, Sellous Ramadhan ameipongeza Azam Media kwa kufanikisha utoaji wa elimu hiyo kwa vijana wengi ambapo mpaka sasa wamewafikia vijana 800 na kuwapa elimu ya namna ya kuwa maofisa bora wa usafirishaji na kusafirisha abiria kwa usalama.

Ofisa Leseni na Usajili LATRA, Denis Daudi, amesema Tanzania inaweza kuwa na rekodi ya ajali sifuri endapo maafisa usafirishaji watazingatia kanuni za usalama barabarani, ikiwemo kuvaa vifaa kinga pamoja na kuendesha kwa mwendo salama.

Ametoa wito kwa wasafirishaji hao kutumia taa salama katika safari zao, huku akionya matumizi ya taa kali ambazo kwa namna moja ama nyingine zimekuwa chanzo cha ajali hasa nyakati za usiku.

Miongoni mwa washiriki wa mafunzo hayo Habibu Ally amesema wamefurahi kupewa elimu hiyo na wataitumia kwa vitendo katika kulinda usalama wa abira na wao wenyewe.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button