DSTV yajipanga Kombe la Dunia

DAR ES SALAAM: FAINALI za Kombe la Dunia 2026 zinatarajiwa kuvunja rekodi mpya duniani baada ya idadi ya timu kuongezeka kutoka 32 hadi 48 huku mechi zikiongezeka kutoka 68 hadi 104 katika mashindano yatakayofanyika kwa mara ya kwanza katika mataifa matatu ya Marekani, Canada na Mexico.

Kutokana na ukubwa huo wa mashindano, kampuni ya DStv kupitia SuperSport imezindua kampeni yake mpya ya “Kila Kitu Kitasubiri” kuelekea michuano hiyo mikubwa zaidi ya soka duniani.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkuu wa Masoko wa DStv, Ronald Shelukindo amesema Kombe la Dunia linaendelea kuwa mashindano makubwa zaidi duniani kutokana na idadi kubwa ya watazamaji wanaofuatilia michuano hiyo.

Shelukindo amesema katika fainali za mwaka 2022 zaidi ya watu bilioni tano walifuatilia mashindano hayo, huku fainali za mwaka 2026 zikitarajiwa kuvunja rekodi zaidi kutokana na maboresho mbalimbali yaliyofanyika.

Amesema kwa upande wa Afrika, bara hilo litawakilishwa na timu 10 jambo linalotarajiwa kuongeza ushindani mkubwa na hamasa kwa mashabiki wa soka.

Katika maboresho hayo, DStv imetangaza kuwa kwa kipindi chote cha mashindano, chaneli ya SuperSport EPLA namba 223 itabadilishwa jina na kuwa SuperSport FIFA World Cup 2026 ambayo itarusha mechi zote hadi kwenye kifurushi cha Bomba.

“Kwa mara ya kwanza mechi za Kombe la Dunia zitaoneshwa hadi kwenye kifurushi cha Bomba ,” amesema Shelukindo.

Aidha, amesema wateja wenye dish tayari watanunua dikoda kwa Sh15,000 huku wanaohitaji kifurushi kamili pamoja na dish wakitakiwa kulipa Sh45,000.

Pia amesema kutakuwa na chaneli maalum kwa Tanzania itakayorusha matangazo kwa lugha ya Kiswahili ili kuwapa urahisi zaidi watazamaji wa ndani kufuatilia mashindano hayo.

Mbali na hayo, Shelukindo alieleza baadhi ya historia za kipekee za Kombe la Dunia ikiwemo tukio la kombe hilo kuibwa na baadaye kupatikana kwa msaada wa mbwa, huku tukio jingine la wizi likitokea mwaka 1983 nchini Brazil.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button