Mashabiki wakutanishwa Liverpool, Chelsea

DAR ES SALAAM: BENKI ya Standard Chartered Tanzania imeandaa tukio maalumu la pamoja la kuonesha moja kwa moja mchezo mkubwa wa Ligi Kuu England kati ya Liverpool FC na Chelsea FC, likiwa na lengo la kuwapa thamani wateja wao.
Tukio hilo lilifanyika katika ukumbi wa Bravo Coco, Dar es Salaam likiwakutanisha wanachama wa Klabu ya Mashabiki wa Liverpool nchini pamoja na wateja maalum wa Standard Chartered, katika mazingira yaliyojaa burudani, mshikamano na furaha ya soka.

Katika kuendeleza ushirikiano wake wa kimataifa na klabu ya Liverpool FC, benki hiyo ilibadilisha ukumbi huo kuwa na mandhari ya Anfield, ikiwa ni pamoja na mapambo maalum, michezo ya maswali kuhusu klabu hiyo pamoja na zawadi mbalimbali zilizoimarisha zaidi uzoefu wa mashabiki.
Akizungumza katika tukio hilo, George Binde, Afisa Mkuu wa Fedha wa Standard Chartered Tanzania, amesema benki hiyo inaendelea kutumia michezo kama daraja la kuimarisha uhusiano na wateja wake.

“Soka lina uwezo wa kipekee wa kuwaunganisha watu. Tunafurahia kuandaa matukio yanayowaleta pamoja wateja wetu na jamii nje ya huduma za kibenki. Tunathamini fursa za kujenga uhusiano wa karibu zaidi na kuacha kumbukumbu za kudumu katika jamii tunazozihudumia,” amesema Binde.
Standard Chartered imeendelea kutumia ushirikiano wake wa kimataifa katika michezo kuleta thamani zaidi kwa wateja wake na jamii, huku ikiimarisha mahusiano kupitia matukio ya aina hiyo katika masoko mbalimbali duniani.



