Mchambuzi wa sera azungumzia changamoto ya maji

Msomi na mchambuzi wa sera za kiuchumi, Aurelia Kamuzora amesema changamoto ya upotevu wa maji na uchakavu wa miundombinu nchini inaweza kupungua kwa kiwango kikubwa iwapo sekta binafsi itapewa nafasi kubwa zaidi katika usimamizi wa miradi ya maji kupitia mfumo wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP).
Prof. Kamuzora alitoa kauli alipokuwa akichangia mada kuhusu sera, haki za kisheria na utekelezaji wa mikataba ya PPP katika Kongamano la Kitaifa kuhusu Sekta ya Maji lililofanyika jijini Dar es Salaam.
Akizungumza kuhusu changamoto za sasa katika sekta ya maji, Profesa Kamuzora alisema wawekezaji binafsi hawawezi kuvumilia upotevu wa rasilimali unaotokana na mabomba yanayovuja, miundombinu chakavu na usimamizi usio na tija, kwa sababu sekta hiyo huongozwa na uwajibikaji na matokeo ya kiuchumi.
Kuingiza nguvu ya sekta binafsi katika usimamizi wa miradi ya maji kutasaidia kujenga nidhamu kubwa ya matumizi ya rasilimali, kuongeza kasi ya matengenezo ya miundombinu na kuboresha huduma kwa wananchi.
Katika hatua nyingine, Prof. Kamuzora alimpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji na kuonesha dhamira ya kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi.
Alisema sera na mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan, umechangia kuongeza imani ya wawekezaji wa ndani na nje, jambo ambalo linaweza kusaidia kukuza uchumi, kuongeza mapato ya Serikali kupitia kodi na kuharakisha maendeleo ya miundombinu nchini.



