Tanzania yaendelea kuimarisha ajenda uchumi wa kidijitali

USWISI – Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki ameongoza ushiriki wa Tanzania katika Maadhimisho ya 3 ya Siku ya Umoja wa Mataifa kuhusu Ulimwengu Pepe ‘3rd UN Virtual Worlds Day’ yanayofanyika Mei 11- 12 Mei, 2026 Geneva, Uswisi.
Ushiriki huo unaonesha nafasi ya Tanzania katika ajenda za kimataifa za maendeleo ya teknolojia mpya, kufuatia nchi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati Tendaji ya Mpango wa Kimataifa wa Akili Unde na Ulimwengu Pepe yaani ‘Global Initiative on AI and Virtual Worlds’ ulioanzishwa kwa ushirikiano kati ya Umoja wa Mataifa (UN) na Shirikisho la Mawasiliano Duniani (ITU).

Katika maadhimisho hayo, Waziri Kairuki alifanya mazungumzo na Naibu Katibu Mkuu wa ITU, Tomas Lamanauskas, na kujadili maeneo mbalimbali ya ushirikiano ikiwemo kuimarisha usimamizi wa teknolojia zinazoibukia, usalama mtandao, usimamizi wa masafa, ubunifu wa TEHAMA pamoja na Maendeleo ya Mifumo ya Umma ya Kidijitali ‘Digital Public Infrastructure’.
Waziri Kairuki aliambatana na mwakilishi wa kudumu wa Tanzania, katika Ofisi ya Umoja wa Mataifa Geneva, Balozi Daktari Abdallah Saleh Possi pamoja na Maafisa Waandamizi kutoka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Ushiriki huu unaunga mkono utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Uchumi wa Kidijitali kwa kuweka mazingira wezeshi ya matumizi ya teknolojia za kisasa, ujenzi wa miji janja (Smart Cities), ubunifu wa kidijitali na huduma jumuishi kwa wananchi.
- Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa mjumbe wa Baraza la Utawala la ITU kwa kipindi cha miaka minne ambapo kupitia ushiriki huo imeweza kunufaika na miradi mbalimbali inayotolewa na ITU kama vile Mradi wa GIGA unaounganisha miundombinu ya mawasiliano katika mashule na uanzishwaji wa vituo vya ubunifu vya kikanda.



