Dk. Mecktridis ahoji hatima ya wakulima waliohamishwa Malinyi

DODOMA: MBUNGE wa Jimbo la Malinyi Dk. Mecktridis Mdaku ametoa hoja Bungeni Jijini Dodoma kwa kuhoji kuhusu hatima ya wananchi wa Malinyi waliohamishwa kutoka katika maeneo yao ya kilimo(Ulanga na Kilombero)na kuwa sehemu ya pori la akiba la Kilombero na kusababisha kuathiri shughuli zao za kilimo cha mpunga kilichokuwa kinawapa kipato.
Amehoji nini mpango wa Serikali wa kuhakikisha wananchi hao waliohamishwa katika maeneo yao wanapata maeneo ya mbadala ya kuendelea na shughuli zao za kilimo.
Akijibu hoja hiyo, wakati wa kuchangia bajeti ya Wizara ya Kilimo, Naibu Waziri wa Kilimo,David Silinde amesema kuwa, kutokana na uamuzi huo, serikali kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo na Tume ya Umwagiliaji imetekeleza mpango wa upanuzi wa mradi wa umwagiliaji wa Itete wenye hekta 850 na bonde la Usangule lenye hekta 12,000 ili kutoa maeneo mbadala kwa wananchi walioathirika na mabadiliko hayo.
Lengo la kuwahamisha wananchi hao lilikuwa kuhifadhi vyanzo vya maji ya Bwawa la mradi wa Mwl. Nyerere, hivyo baadhi ya wananchi waliathirika baada ya maeneo yao kuingia kwenye hifadhi ya pori la Kilombero.
Amesema kuwa, kwa sasa ujenzi wa mradi wa umwagiliaji Itete umefikia asilimia 64, na upembuzi yakinifu wa bonde la Usangule umefikia asilimia 84. Miradi hii ikikamilika itaonufaisha wakazi zaidi ya wakulima 9,000 na kuleta tija ya kilimo kwao wote.
Pia amesema Serikali itaendelea kutoa elimu ya kilimo bora cha mpunga ili kuwawezesha kuongeza tija katika kilimo chao.



