‘Mradi wa barabara Tarime – Mugumu uzingatie ubora’

MARA: KATIBU wa NEC Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Kenan Kihongosi amesisitiza mradi wa barabara ya Tarime hadi Mugumu ujengwe ukizingatia ubora ili kuepusha uharibifu wa mapema wa barabara baada ya kukamilika.
Kihongosi ameeleza hayo leo Mai 16,2026 alipotembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa barabara hiyo ambayo inagharimu zaidi ya Sh bilioni 81 katika utekelezaji wake, iliwa ni muendelezo wa ziara yake ya kikazi mkoani Mara.

Akizungumza baada ya kukagua mradi huo Kihongosi amepongeza Wakala wa Barabara (TANROADS) kwa usimamizi mzuri wa barabara hiyo, huku akimtaka mkandarasi anayetekeleza barabara hiyo kuhakikisha ujenzi unakamilika kwa wakati ili wananchi waanze kunufaika na huduma ya usafiri na uchumi.
Pia amesisitiza mradi huo ujengwe kw akuzongatia ubora ili kuepusha usumbufu unaotokana na uharibifu wa mapema mara baada ya barabara kukamilika, akisisitiza kuwa chama hakitoweza kuvumilia kuona barabara inajengwa kwa gharama lakini chini ya viwango.

“Wananchi wanahitaji kuona barabara inakamilika, hawahitaji kuona mitambo pekee, mradi huu upo kwenye ilani ya uchaguzi hivyo lazima ukamilike kwa wakati. Pia Chama hakiwezi kuvumilia kuona barabara inayojengwa kwa gharama kubwa inaharibika ndani ya miaka michache,” amesema.
Awali, akiwasilisha taarifa ya mradi huo, Mhandisi Deus Julius akimuwakilisha Mkurugenzi wa Tanroads amesema mradi huo unatekelezwa kwa awamu mbili.

Amesema awamu ya kwanza kutoka Mogabiri hadi Nyamongo yenye urefu wa kilomita 25 inatekelezwa na kampuni ya Nyanza Road Works ambapo utekelezaji umefikia asilimia 64 huku kilomita 15 zikiwa tayari zimewekewa lami.
Aidha amesema awamu ya pili ya kilomita 65.5 kutoka Nyamongo hadi Mugumu inatekelezwa na kampuni ya Stecol Corporation kwa gharama ya zaidi ya Sh bilioni 81.
Barabara hiyo imetajwa kuwa ni kiungo muhimu kinachounganisha Wilaya za Tarime, Serengeti na maeneo ya mpakani mwa Kenya huku ikiwa na mchango mkubwa katika usafirishaji wa watalii wanaokwenda kwenye hifadhi pamoja na mazao ya biashara yanayolimwa katika ukanda huo.



