MORUWASA yapewa dhamana kupunguza upotevu maji

MOROGORO:WIZARA ya Maji imeitaka Bodi mpya ya 10 ya Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Morogoro (MORUWASA), kuanza kazi kwa kusimamia mapambano dhidi ya mivujo ya maji ili kuongeza ufanisi wa huduma endelevu na yenye uhakika na kupunguza upotevu wa maji unaosababisha hasara kwa mamlaka.
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mhandisi Mwajuma Waziri amesema hayo katika hotuba yake ya kumkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima kuzindua bodi hiyo mjini Morogoro.

Mhandisi Waziri amesema usimamizi madhubuti wa miundombinu ya maji ni muhimu katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, endelevu na yenye uhakika.
Hivyo amewataka wajumbe wa bodi kufanyia kazi maono ya Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, kwa kuweka mkazo katika maeneo matatu muhimu ambayo ni pamoja na matumizi ya teknolojia za kisasa katika utoaji wa huduma za maji.
Ametaja maeneo mengine ni kuimarisha rasilimali watu pamoja na kutafuta na kutumia vyanzo mbadala vya fedha ili kuongeza ufanisi na kuimarisha utekelezaji wa miradi ya maji.

Katibu Mkuu pia amewataka watumishi wa MORUWASA kutoa ushirikiano wa kutosha kwa bodi mpya ili kuiwezesha kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kufikia malengo yaliyowekwa kwa manufaa ya wananchi.
“Pia niwapongeze wajumbe wa bodi mpya hii na ninatarajia bodi itafanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na wafanyakazi wa mamlaka pamoja na kusimamia miradi yote inayotekelezwa na mamlaka na kuhakikisha kuwa inakuwa na ubora unaotakiwa,” amesema Mhandisi Waziri.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Malima, kwenye hotuba yake ya uzinduzi ameitaka bodi hiyo kuendeleza mafanikio yaliyoanzishwa na watangulizi wao na kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama kwa uhakika.

“Nina imani kubwa na utendaji kazi wa menejimenti iliyopo pamoja na bodi yake iliyozinduliwa kwa sababu ina watu wenye uwezo,” amesema Malima.
Malima amesema anaamini kuwa bodi hiyo itawajibika kikamilifu kwenye utendaji wao kutokana na uwezo walionao wa kusaidia kutatua changamoto zilizopo kwenye mamlaka hiyo.
Kwa upande wake Mwenyekiti mpya wa bodi hiyo, Profesa Moses Warioba amesema bodi ipo tayari kufanya kazi kwa bidii na kufuata miongozo ikitambua jukumu la maji katika jamii ni la watu wote.
“Bodi hii tunatarajia tutapata ushirikiano kwa mamlaka na taasisi zote zinazojihusisha na masuala ya maji pamoja na jamii kwa ujumla ili kufanikisha malengo tuliyojiwekea,” amesema Profesa Warioba.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa mamlaka hiyo, CPA Sais Kyejo alisema mamlaka inaendelea kutekeleza miradi 12 ya maji ya muda mfupi yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 71.6 kwa lengo la kuboresha huduma ya maji katika maeneo mbalimbali yanayosimamiwa na MORUWASA mkoani humo.

Mkurugenzi Mtendaji huyo ametaja changamoto kubwa kuliko zote ni upotevu wa maji yasiyolipiwa ambapo kwa sasa mamlaka inapoteza wastani wa asilimia 50 na kusababisha mapato kupatikana madogo yasiyokidhi uendeshaji.



