CCM: Siasa zituunganishe zilete upendo, umoja

BUNDA: CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema siasa zitumike kuunganisha watu, zilete upendo na umoja na wazikatae siasa za chuki na wanasiasa wanaotafuta umaarufu wa kisiasa kwa kutumia matukio mbalimbali kuchochea migogoro na kuvuruga umoja uliopo.

Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM), Kenani Kihongosi ameeleza hayo leo Mei 17,2026 alipokuwa akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya CCM kata ya Kabarimi Wilaya ya Bunda mkoani Mara.

Akizungumza katika mkutano huo Kihongosi amesema siasa zinapaswa kuunganisha wananchi, kuleta upendo na kuimarisha umoja badala ya kutumiwa kama njia ya kugawa jamii.

“Siasa zituunganishe, siasa zilete upendo, siasa zilete umoja msije na haya mambo, lazima tuambizane. Kataeni siasa za hovyo na wanasiasa wanaotafuta umaarufu wa kisiasa,” amesema.

Amedai kuwa baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakitumia matukio mabaya kama mitaji ya kisiasa huku wakichochea wananchi dhidi ya serikali na vyombo vya ulinzi na usalama, amewasisitiza wasibebe ajenda za watu wasizozijua.

“Siasa za hivi leo zina maslahi wanatafuta umaarufu wa kisiasa na wanachochea mambo mabaya, wanapotokea wanasema ‘tumepigwa, tumeumizwa,ni kweli wameumia?, lakini matukio hayo yanageuzwa mtaji wa kisiasa,” amesema.

Aidha, aliwataka wananchi wa Bunda kutokubeba agenda za kisiasa zinazoweza kuleta migawanyiko katika jamii akisisitiza kuwa hakuna mtu aliyezaliwa na chama cha siasa.

“Hakuna aliyezaliwa na chama cha siasa hapa, ukiona mtu anagombana kwa sababu ya siasa huyo ni mshamba wa kisiasa,” amesema.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button