TFS kujenga kiwanda cha uchakataji mazao ya nyuki

SINGIDA: WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) unatarajia kujenga kiwanda kipya na uwekaji mitambo ya kisasa kwa ajili ya kuchakata mazao ya nyuki ili kuwezesha kukidhi mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi la asali.
Kiwanda hicho kipya kitajengwa wilayani Manyoni, Mkoa wa Singida ambako kuna kiwanda kidogo cha uchakataji kinachohudumia Kanda ya Kati inayojumisha mikoa ya Singida, Manyara na Dodoma ambacho kinatarajiwa kugharimu zaidi ya Sh milioni 200 .
Mhifadhi Mkuu Daraja la Pili wa TFS , Claudia Kinabo amesema hayo alipozungumzia mikakati ya uzalishaji wa mazao ya nyuki ikiwemo asali katika kanda hiyo na namna ilivyojioanga kwenye maadhimisho ya Siku ya Nyuki Duniani Mei 20 mwaka huu ambapo kitaifa ya kifanyika mkoani Tabora.
Kinabo ambaye ni msimamizi wa kitengo cha Ufugaji Nyuki Kanda ya Kati alisema Wakala huo umetenga bajeti kwa ajili ya kujenga kiwanda kikubwa zaidi ya ukataji wa mazao ya nyuki ambapo kwa sasa kipo kiwanda kidogo katika kituo cha Wilaya ya Manyoni.

“Ujenzi kwa maana ya upanuzi huu wa kiwanda cha Manyoni utakuwa na mchango mkubwa katika kukuza sekta ya asali na kuongeza uzalishaji katika eneo hili,” amesema Kinabo.
Kinabo amesema Kanda yaKati unaendelea kuwa miongoni mwa maeneo yanayoongoza kwa uzalishaji wa asali chini ya TFS kwa sababu ina mazingira mazuri ya misitu yanayofaa kwa ufugaji nyuki.
Amesema kuwa Kanda hiyo una mashamba makubwa matano ya nyuki yaliyopo katika wilaya za Singida na Kondoa, maeneo yanayojulikana kwa mazingira mazuri ya ufugaji nyuki na uzalishaji wa asali bora.
Naye, Mhifadhi Nyuki Shamba la Nyuki Manyoni, Mrina Robert amesema kiwanda cha kuchakata mazao ya nyuki kimekuwa kikichakata mazao hayo kutoka wilaya mbalimbali za Kanda ya Kati pamoja na asali za wadau mbalimbali .
Mrina amesema kiwanda cha sasa licha ya kuendelea kuchakata mazao ya nyuki kikiwa na uwezo wa kuchakata kilo 500 kwa saa nane kwa siku.
Amesema kutokana na mahitaji makubwa na mtambo uliopo ni mdogo pamoja na jengo, wakala katika bajeti yake umejipanga kujenga jengo kubwa la kiwanda na kuweka mitambo mikubwa nay a kisasa zaidi ya kuchakata mazao ya nyuki kwa maana ya asali, nta na mengine.
Mrina amesema kiwanda hicho kipya kitachangia kuongeza kasi ya uchakataji wa asali na kutoa ushawishi kwa wadau wenye mashamba ya nyuki kuleta mazao yao kuchakatwa.
Kwa upande wake, Mhifadhi Mkuu na Msaidizi wa Kamanda wa TFS Kanda ya Kati anayeshughulikia Dawati la Mipango na Masoko, Ignas Lupala alisema kwa mwaka wa fedha wa 2024/2025 lengo lilikuwa kuzalisha tani 20 za mazao ya nyuki na hadi kufikia msimu ulipomalizika zilizalishwa tani 16.5 za asali.
Lupala amesema kwa mwaka wa fedha 2025/2026 Kanda hiyo imeweka lengo la kuvuna jumla ya tani 21 za asali na bado msimu wa uvunaji unaendelea na mikakati mbalimbali imewekwa ya uzalishaji mazao ya nyuki kwa wingi yanafikiwa kila mwaka.



