CMSA: Taasisi za kifedha zifuate miongozo ya uwekezaji

DAR ES SALAAM: MAMLAKA ya Masoko ya Mitaji na Dhamana CMSA, imezitaka taasisi za kifedha zinazotoa huduma ya uwekezaji wa hisa kupitia hatifungani ambazo zinatolewa na taasisi hizo kufuata muongozo wa huduma za dhamana zilizo chini ya mamlaka hiyo na Benki Kuu.
Kwa mujibu wa majarida mbalimbali ya kiuchumi ulimwenguni uwekezaji wa hatifungani ni miongoni mwa eneo ambalo linatajwa kuwa na usalama zaidi ikilinganishwa na uwekezaji wa kifedha kwenye maeneo mengine.
Licha ya usalama huo ajenda ya kuzingatia sheria ya usimamizi wa utoaji wa huduma za kifedha bado inapaswa kutiliwa mkazo kwa kampuni na taasisi za kifedha kwa kufuata muongozo wa Benki Kuu ya Tanzania BOT, pamoja na Wizara ya Fedha.
Akiwa kwenye uzinduzi wa batifungani ya Taasisi ya Huduma za Kifedha ya iTrust ambayo inatoa faida ya asilimia 13 yenye ukomavu wa miaka minne, Mkurugenzi wa Utafiti, Sera na Mipango wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana CMSA, Alfred Mkombo, amesema taasisi zinazotoa huduma za kifedha ikiwemo mauzo ya Hatifungani zinazo wajibu wa kuzingatia sheria ili kuweza kutoa huduma hizo kwa usawa.
Awali, Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa la Dar es Salaam DSE, Peter Nalitolela amesema uzinduzi wa hatifungani hizo wenye thamani ya zaidi ya kiasi cha Sh Bilioni 15 unatarajiwa kuwa sehemu ya kukuza Sekta ya soko la hisa nchini.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa I trust Finance Faiz Arab amesema dhamana imeundwa ili kuvutia wawekezaji wengi na kikomo cha chini cha uwekezaji ni sh.500,000 jambo linalouwezesha kupatikana kwa wawekezaji binafsi na taasisi.



