Serikali kufanya mapitio sheria za uhifadhi

WAZIRI Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba amesema Serikali ina mpango wa kufanya mapitio ya sheria zinazohusiana na uhifadhi kwa lengo la kuimarisha mahusiano kati ya maeneo ya hifadhi na jamii zinazozunguka maeneo hayo.
Akichangia hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii jana, Dk Mwigulu alisema serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ni Serikali inayowajibika kwa Watanzania na kuwahidi wabunge kuwa hoja za wabunge zitafanyiwa kazi kwa kufanya mapitio ya sheria za uhifadhi na mipaka ya maeneo ya hifadhi.
“Kwa hoja hizi ambazo zimejitokeza kuanzia kwenye michango ya wabunge na zile zilizojitokeza katika kipindi ambacho Bunge lako limekaa kama Kamati, Serikali tumezipokea,” amesema.
Dk Mwigulu alisema tayari Rais Samia ameelekeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Wizara ya Katiba na Sheria kufanya mapitio ya sheria hizo.
Alisema mapitio hayo yatahusisha kuangalia upya sheria za uhifadhi pamoja na sheria zinazohusu mipaka ya maeneo ya hifadhi, hususan katika maeneo ambayo wananchi hawana uelewa wa mipaka halisi.
“Tutafanya kazi hiyo ili wananchi wajue hasa mpaka ni wapi,” amesema.
Dk Mwigulu alisema pia Serikali pia itafanyia kazi suala la mahusiano kati ya wananchi na maeneo ya hifadhi kwa kuangalia upya baadhi ya vifungu vya sheria vinavyohusu adhabu.
“Kwa sasa kuna baadhi ya adhabu zinazofanana kwa makosa yenye uzito tofauti, anayekamatwa na mkaa na aliyebeba meno ya tembo wanapata adhabu inayofanana. Yule aliyelima mazao yake kwenye hifadhi na anayefanya ujangili wote wanaonekana sawa kisheria, hivyo tutazifanyia kazi sheria ili kuboresha ustawi wa maisha ya Watanzania pamoja na kuimarisha uhifadhi na sekta ya utalii nchini.”
Akichangia, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamad Hassan Chande alisema Serikali haitawavumilia watumishi wanaokwenda kinyume na maadili ya utumishi wa umma, na kuwa tayari imechukua hatua ya kuwasimamisha kazi watendaji 17 na wengine kuwashusha vyeo.
“Na hapa ni kuahidi, Serikali haitawavumilia watumishi yeyote wanaokwenda kinyume na maadili ya utumishi wa umma. Sisi kama viongozi hatutokuwa tayari kuona mwananchi yeyote anapata shida.”
Kuhusu hoja ya malikale, Chande alikiri kuwa pamoja na juhudi za kutambua maeneo ya malikale, bado baadhi ya maeneo hayajafikiwa.
“Serikali imefanya kazi kubwa sana ya kupitia maeneo ya malikale katika vivutio mbalimbali nchini, lakini kweli baadhi ya maeneo hatujayafikia. Serikali imeandaa timu inayopita kila sehemu kufanya utafiti ili kubaini maeneo zaidi na yaingie katika orodha.”



