Serikali yaweka mkono walioathiriwa na wanyamapori

DODOMA; WAZIRI wa Maliasili na Utalii,  Dk Ashatu Kijaji amesema Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia kuiongezea wizara hiyo Sh bilioni sita kwa ajili ya kulipa kifuta jasho na kifuta machozi kwa wananchi walioathiriwa na wanyamapori wakali na waharibifu.

Akijibu hoja za wabunge waliochangia hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka 2025/26, Dk Kijaji alisema tayari serikali imepitisha Sh bilioni 12.3 kwa ajili ya malipo hayo ambapo kati ya Januari hadi Mei 17 mwaka huu, zaidi ya Sh bilioni tisa zimeshatumika kuwalipa waathirika huku Sh bilioni 2.2 zimetolewa mwishoni mwa wiki ili kuendelea na malipo kwa waathirika.

“Rais Samia Suluhu Hassan ameielekeza wizara tuongezewe Sh bilioni sita ili wale wote ambao hawakulipwa kuanzia mwaka 2023 waweze kufikiwa au angalau tufikie asilimia 70 ya kuwashika mkono wananchi walioathirika na wanyamapori wakali na wahalibifu,” amesema.

Dk Kijaji alisema serikali imeboresha mfumo wa malipo kwa kutumia akaunti za benki na simu za wananchi moja kwa moja ili kuondoa ucheleweshaji na matumizi yasiyo sahihi ya fedha.

Hata hivyo, alisema changamoto bado ipo kutokana na baadhi ya wananchi kuwasilisha akaunti zisizofanya kazi au namba za simu ambazo hazilingani na majina ya walipaji jambo linalokwamisha mfumo kufanya malipo na kuwaomba wabunge kuwahamasisha wananchi katika majimbo yao kuhakikisha wanatumia taarifa sahihi ili waweze kulipwa kwa wakati.

Kuhusu ongezeko la migogoro kati ya wananchi na wanyamapori, Dk Kijaji alisema wizara imefanya tafiti kubaini chanzo cha tatizo hilo ambapo matokeo yanaonesha ongezeko la watu wanaosogea karibu na maeneo ya hifadhi.

Alisema pamoja na hoja kuwa idadi ya tembo imeongezeka, sensa ya mwaka jana inaonesha Tanzania ina tembo 66,000 ikilinganishwa na zaidi ya tembo 300,000 waliokuwepo mwaka 1961 wakati wa uhuru.

“Tatizo kubwa ni ongezeko la watu na shughuli za kibinadamu kusogea karibu na hifadhi. Wanyama nao wanatafuta chakula na maji hivyo kuingia kwenye maeneo ya wananchi,” alisema.

Dk Kijaji alisema serikali imeandaa mkakati mpya wa miaka 10 wa kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu utakaoanza kutekelezwa kuanzia mwaka 2027 hadi 2037.

Alisema mkakati huo unahusisha kuongeza uzio wa umeme katika maeneo ya hifadhi, kununua helikopta za kusaidia kurejesha wanyama porini pamoja na matumizi ya teknolojia ya mikanda maalumu ya kufuatilia mienendo ya tembo.

Kwa sasa alisema serikali imenunua mikanda 76 ambayo imefungwa kwa tembo viongozi ili kusaidia kufuatilia makundi yao na kutoa tahadhari mapema wanapokaribia makazi ya wananchi.

Aidha, alisema serikali inaendelea kuchimba mabwawa ndani ya hifadhi ili kuhakikisha wanyama wanapata maji huko huko na kupunguza uwezekano wa kutoka nje ya maeneo yao.

Katika hatua nyingine, Dk Kijaji alikiri kuwepo changamoto katika utendaji wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) lakini akaahidi maboresho makubwa yatafanyika ndani ya kipindi cha miezi sita.

Alisema serikali imeendelea kuongeza fedha za bodi hiyo ambapo mwaka huu imepokea zaidi ya asilimia 77 ya fedha zilizoidhinishwa na Bunge kwa ajili ya shughuli za kutangaza utalii.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button