Kadogosa ataka nguvu zaidi ukarabati miundombinu ya barabara

MBUNGE wa Bariadi Vijijini, Masanja Kadogosa (CCM), amesema sehemu kubwa ya miundombinu ya barabara imeanza kufikia muda wake wa mwisho wa matumizi, hivyo kuishauri serikali kuongeza nguvu katika ukarabati wa barabara hizo.

Akichangia hotuba ya Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Mbunge Kadogosa amesema barabara nyingi zilizojengwa miaka ya nyuma sasa zinahitaji matengenezo makubwa kutokana na uchakavu.
Mbunge huyo amesema miaka michache ijayo, taifa linaweza kukumbwa na changamoto kubwa ya miundombinu iwapo ukarabati hautapewa kipaumbele sambamba na ujenzi wa barabara mpya.
Amesema serikali inapaswa kuhakikisha fedha za matengenezo zinaongezwa, ili kulinda uwekezaji mkubwa uliofanyika katika sekta hiyo, akifafanua kuwa matengenezo ya mara kwa mara ni muhimu zaidi kuliko kusubiri barabara ziharibike kabisa ndipo hatua zichukuliwe.
Amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi kubwa za kuboresha miundombinu nchini pamoja na Waziri wa Ujenzi kwa kuendelea kusimamia mipango mbalimbali ya maendeleo ya barabara inayotekelezwa katika maeneo tofauti nchini.
Kuhusu Mkoa wa Simiyu amesema bado unahitaji kupewa kipaumbele maalumu kutokana na kuwa miongoni mwa mikoa mipya inayohitaji mtandao mkubwa wa barabara, ili kuchochea maendeleo ya wananchi wake na kukuza shughuli za kiuchumi.



