DIPLOMASIA YA MADINI

Jinsi diplomasia ya uchumi ilivyoifanya Tanzania kuwa kitovu kipya cha uwekezaji wa madini Afrika

MAHENGE — Kabla hata mgodi wa kinywe wa Mahenge haujaanza kuzalisha tani moja ya madini, dalili za mabadiliko tayari zinaonekana katika Wilaya ya Ulanga. Zaidi ya wananchi 1,200 waliopisha mradi wamelipwa fidia, ofisi za vijiji zimejengwa, shule zimekarabatiwa, visima vya maji vimechimbwa, huku maandalizi ya kupeleka umeme wa kilovoti 220 kutoka Ifakara hadi Mahenge na kuboresha mtandao wa barabara yakiendelea.

Kilichokuwa kinaonekana kama uwekezaji wa mgodi mmoja sasa kinaanza kubadili sura ya uchumi wa eneo hilo. Hata hivyo, simulizi ya Mahenge ni sehemu ndogo ya mabadiliko makubwa yanayoendelea Tanzania, ambako sekta ya madini imekuwa moja ya nguzo za diplomasia ya uchumi katika kipindi ambacho dunia inashindania upatikanaji wa madini muhimu ya kimkakati yanayotumika katika magari ya umeme, nishati jadidifu, vifaa tiba na teknolojia za kisasa.

Mabadiliko hayo yalidhihirika Mei mwaka huu katika Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji wa Madini (MICE 2026) uliofanyika Nairobi, Kenya. Badala ya Tanzania kujieleza yenyewe, mawaziri wa madini kutoka Kenya, Somalia na Sudan Kusini waliitaja hadharani kuwa moja ya nchi wanazojifunza kutoka katika usimamizi wa sekta ya madini, sera za uongezaji thamani na ushirikishwaji wa wachimbaji wadogo.

Kauli hizo zilionyesha mabadiliko ya namna Tanzania inavyoanza kutazamwa katika ukanda wa Afrika Mashariki. Kwa mara nyingine, nchi haikutambulishwa kwa utajiri wa madini iliyonayo pekee, bali kwa juhudi zake za kutumia sera na diplomasia kuvutia uwekezaji, teknolojia na ushirikiano wa kimataifa.

Mapinduzi ya Diplomasia ya Madini

Mabadiliko hayo yanakuja wakati ushindani wa kimataifa wa madini muhimu ukizidi kushika kasi. Mataifa makubwa yanaongeza uwekezaji, mikataba ya ununuzi wa madini na ushirikiano wa kimkakati ili kuhakikisha yanapata uhakika wa malighafi zinazohitajika kwa teknolojia za baadaye.

Lakini kuvutia wawekezaji pekee hakutoshi. Ili kuongeza nafasi yake katika ushindani wa madini muhimu, Tanzania inalazimika kwanza kuelewa kwa kina rasilimali ilizonazo. Kwa sasa takribani asilimia 16 pekee ya eneo la Tanzania limefanyiwa utafiti wa kina wa kijiolojia, hali inayomaanisha kuwa sehemu kubwa ya rasilimali za nchi bado haijafahamika kikamilifu.

Katika ziara rasmi ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini Urusi mwezi Juni mwaka huu, ushirikiano katika sekta ya madini haukujikita kwenye uwekezaji pekee.

“Mazungumzo yalielekezwa pia katika utafiti wa kijiolojia, uchoraji wa ramani za madini, teknolojia za kisasa, mafunzo kwa wataalamu wa Kitanzania na kuimarisha ushirikiano kati ya Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) na taasisi za utafiti za Urusi,” anasema Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo.

“Tanzania itaendelea kutumia diplomasia ya uchumi kuvutia uwekezaji wenye tija, kuhamisha teknolojia na kuongeza thamani ya rasilimali zetu ili ziwe chachu ya maendeleo endelevu na ajira kwa wananchi.”

Kauli hiyo inaonyesha kuwa diplomasia ya Tanzania katika sekta ya madini sasa haihusu tena kuvutia mitaji pekee. Inahusu pia kujenga maarifa, teknolojia na uwezo wa kitaifa wa kugundua rasilimali ambazo bado hazijafikiwa.

Kwa mujibu wa wachambuzi wa sekta hiyo, ushindani wa sasa hauhusu tena nani anamiliki mgodi pekee, bali nani anadhibiti mnyororo wa thamani wa madini hayo—kuanzia utafiti wa kijiolojia, uchimbaji, uchakataji, usafishaji hadi utengenezaji wa bidhaa za mwisho.

Katika mazingira hayo, Tanzania imeibuka kama moja ya nchi zenye fursa kubwa kutokana na uwepo wa madini muhimu kama kinywe, nikeli, madini adimu ya ardhini (Rare Earth Elements–REE) na helium.

Mwelekeo huo umepewa uzito zaidi na Rais Samia ambaye katika Mkutano wa 29 wa Kimataifa wa Uchumi wa St. Petersburg (SPIEF 2026) nchini Urusi aliitaja sekta ya madini kuwa moja ya maeneo muhimu ya ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na dunia.

“Tunataka kutoka katika kuwa wauzaji wa malighafi na kuwa wazalishaji wa bidhaa zilizokamilika. Tunakaribisha washirika kuwekeza nasi katika viwanda vitakavyofungua thamani halisi ya rasilimali zetu za madini,” amesema Rais Samia.

Wachambuzi wanasemaje

Uchambuzi wa taasisi ya kimataifa ya Natural Resource Governance Institute (NRGI), Tanzania ina mkusanyiko mpana wa madini muhimu yanayohitajika katika mabadiliko ya dunia kuelekea matumizi ya nishati safi. Miongoni mwa madini hayo ni kinywe, nikeli, REE, helium, cobalt na shaba, ambayo yanatarajiwa kuwa msingi wa teknolojia za kizazi kijacho.

Uchambuzi huo unaonyesha pia jinsi mwelekeo wa uwekezaji ulivyobadilika ndani ya kipindi cha miaka miwili iliyopita. Mwaka 2005 karibu asilimia 90 ya leseni za utafutaji wa madini nchini zilikuwa zikielekezwa kwenye dhahabu. Kufikia mwaka 2025, karibu asilimia 70 ya leseni hizo zilikuwa zimehamia kwenye madini muhimu, ishara kwamba wawekezaji wanaelekeza mitaji yao kwenye rasilimali zinazohitajika katika uchumi wa nishati safi.

Kwa mchambuzi wa sekta ya madini Abdulrazak Yahya, mabadiliko hayo yanaipa Tanzania nafasi ya kipekee katika ushindani wa kimataifa.

“Upekee wa Tanzania unatokana na mchanganyiko wa kinywe, nikeli na madini adimu ya ardhini. Nchi nyingi zina aina moja au mbili za madini muhimu, lakini Tanzania ina rasilimali kadhaa zinazohitajika kwa wakati mmoja katika teknolojia za betri, magari ya umeme na nishati mbadala,” anasema.

Anasema miradi ya kinywe, Mradi wa Nikeli wa Kabanga na Mradi wa Ngualla wa Madini Adimu ya Ardhini inaipa Tanzania nafasi ya kushiriki katika mnyororo wa thamani wa teknolojia mpya duniani.

Hata hivyo, anaonya kuwa ushindani bado ni mkubwa kutoka nchi kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Zimbabwe, Namibia na Msumbiji. Kwa hiyo, mafanikio ya Tanzania yatategemea uwezo wa kuendelea kuboresha sera, miundombinu, mazingira ya uwekezaji na uongezaji thamani wa madini.

Diplomasia hiyo imeungwa mkono na hatua za kisera zilizochukuliwa katika miaka ya hivi karibuni. Serikali imeendelea kufanya mazungumzo na wawekezaji wa kimataifa huku ikisisitiza kuwa madini mengi yaongezewe thamani nchini kabla ya kusafirishwa nje. Lengo ni kuongeza mapato ya taifa, ajira, uhamishaji wa teknolojia na ushiriki wa Watanzania katika hatua nyingi zaidi za mnyororo wa thamani wa sekta ya madini.

Moja ya ishara za mkakati huo ilionekana Mei 2026 wakati Rais Dk. Samia Suluhu Hassan alipokutana Ikulu Chamwino na viongozi wa Kampuni ya Perseus Mining Limited na Sotta Mining Corporation Limited kujadili maendeleo ya uwekezaji katika sekta ya madini. Kwa wachambuzi wa uchumi, mikutano hiyo haikuwa ya kawaida ya uwekezaji, bali sehemu ya diplomasia ya uchumi inayolenga kuiweka Tanzania katika ramani ya mataifa yanayonufaika na ongezeko la mahitaji ya madini muhimu duniani.

Miezi michache baada ya mazungumzo hayo, matokeo ya mkakati huo yalianza kujitokeza. Kampuni ya Perseus Mining ilitangaza kuwa ujenzi wa Mgodi wa Dhahabu wa Nyanzaga wenye thamani ya dola za Marekani milioni 523 umefikia hatua kubwa, huku uzalishaji ukitarajiwa kuanza Januari 2027. Serikali ya Tanzania inamiliki asilimia 20 ya hisa katika mradi huo, ambao tayari umezalisha zaidi ya ajira 3,000 katika kipindi cha ujenzi.

Tahadhari ni ipi

Hata hivyo, simulizi ya sekta ya madini nchini sasa haijajikita tena kwenye dhahabu pekee. Kadiri dunia inavyoongeza matumizi ya magari ya umeme, mifumo ya kuhifadhi nishati na teknolojia za kisasa, mahitaji ya kinywe, nikeli, helium na madini adimu ya ardhini yanaendelea kuongezeka kwa kasi.

Shirika la Kimataifa la Nishati (IEA) linaeleza kuwa mabadiliko kuelekea matumizi ya nishati safi yataongeza kwa kiwango kikubwa mahitaji ya madini hayo katika miongo ijayo, jambo linalozifanya nchi zenye rasilimali hizo kuwa sehemu muhimu ya uchumi wa dunia.

Ndani ya mazingira hayo ya ongezeko la mahitaji ya madini muhimu, Tanzania imeharakisha utekelezaji wa miradi mikubwa katika maeneo mbalimbali ya nchi, ikilenga kujikita kwenye mnyororo wa thamani wa madini badala ya kusafirisha malighafi pekee.

Wilayani Ruangwa, mkoani Lindi, Serikali imeingia ubia na Kampuni ya Lindi Jumbo Limited kuendeleza mradi mkubwa wa kinywe. Madini hayo ni malighafi muhimu katika utengenezaji wa anode, sehemu ya msingi katika betri za lithium-ion zinazotumika kwenye magari ya umeme na mifumo ya kuhifadhi nishati.

Waziri wa Madini Anthony Mavunde anasema mwelekeo wa Serikali ni kuhakikisha Tanzania inanufaika zaidi na rasilimali zake kupitia uongezaji thamani ndani ya nchi.

“Hakuna madini yatakayotoka nje ya nchi bila kuongezwa thamani. Huo ndiyo mwelekeo wa Serikali na tayari wawekezaji wameuelewa,” anasema.

Kauli hiyo ilitolewa Juni 27, 2026 wakati wa uzinduzi wa maandalizi ya Mkutano wa Saba wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini Tanzania (TMIC 2026), ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha diplomasia ya madini na kuvutia uwekezaji wa kimkakati.

Mbali na Lindi, Wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro imeibuka kuwa kitovu kingine cha uwekezaji wa kinywe kupitia miradi ya Faru Graphite na Duma Graphite chini ya Kampuni ya TanzGraphite.

Kwa mujibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga, uwekezaji huo unatarajiwa kuzalisha takribani ajira 900 za moja kwa moja na zaidi ya 4,000 zisizo za moja kwa moja. Aidha, miradi hiyo imechochea maboresho ya miundombinu ikiwemo barabara na usambazaji wa umeme wa kilovoti 220 kutoka Ifakara hadi Mahenge.

Kwa wakazi wa Mahenge, mabadiliko yameanza kuonekana hata kabla ya uzalishaji rasmi kuanza. Zaidi ya wananchi 1,200 waliopisha mradi wamelipwa fidia, huku kampuni zikiendelea kutekeleza miradi ya kijamii kama sehemu ya maandalizi ya uwekezaji.

Afisa Uhusiano wa Faru Graphite, Jacqueline Mushi, anasema kampuni imeamua kuhakikisha jamii inanufaika sambamba na maendeleo ya mradi.

“Kabla uzalishaji haujaanza, tayari tumeanza kutekeleza miradi ya maendeleo katika jamii, ikiwemo ujenzi wa ofisi za vijiji, ukarabati wa shule na miradi ya maji. Lengo ni kuhakikisha jamii inashiriki na kunufaika na uwekezaji huu,” anasema.

Mabadiliko hayo yanaonekana pia katika maisha ya wananchi wa kawaida. Biashara ndogo ndogo zimeongezeka, vijana wengi wamepata ajira za muda na shughuli za kiuchumi zimechukua mwelekeo mpya kutokana na ongezeko la watu na vifaa vya ujenzi katika eneo hilo.

Mmoja wa wakazi wa Mahenge, Rehema Mhando, anasema mazingira ya biashara yamebadilika kwa kasi.

“Tulikuwa tunaona magari yanapita tu. Sasa biashara imeongezeka, vijana wamepata ajira na tunaanza kuona mabadiliko ambayo hatukuyategemea miaka michache iliyopita,” anasema.

Wakati huo huo, Mkoa wa Njombe unajiandaa kuwa mmoja wa wazalishaji wakubwa wa madini adimu ya ardhini kupitia Mradi wa Ngualla, unaohusisha madini ya Neodymium na Praseodymium, yanayotumika kutengeneza sumaku zenye nguvu kwa mitambo ya upepo, magari ya umeme na vifaa vya teknolojia ya juu.

Nao Mkoa wa Songwe umeingia katika ramani ya dunia kupitia mradi wa helium unaoendelezwa na Helium One Global kwa ubia na Serikali. Helium ni gesi adimu inayotumika katika mashine za MRI, utengenezaji wa semiconductors, satelaiti na teknolojia za anga.

Mustakabali wa Tanzania katika Uchumi wa Madini Muhimu

Pamoja na mafanikio hayo, wataalamu wanaonya kuwa diplomasia ya madini pekee haitoshi bila uimarishaji wa taasisi na usimamizi bora wa rasilimali.

Mkurugenzi Mtendaji wa HakiRasilimali, Adam Anthony, anasema ukuaji wa sekta ya madini muhimu unapaswa kuendana na uwazi na uwajibikaji ili kuhakikisha rasilimali zinawanufaisha wananchi kwa muda mrefu.

“Ingawa Tanzania bado haijaanza uzalishaji mkubwa wa baadhi ya madini muhimu kama lithiamu, uzoefu wa sekta ya dhahabu unaonyesha umuhimu wa kujenga mifumo imara ya utawala kabla uwekezaji haujakua kwa kasi,” anasema.

Anasema bila mifumo madhubuti, ongezeko la uwekezaji linaweza kuleta changamoto kama migogoro ya ardhi, upotevu wa mapato na utegemezi wa kuuza malighafi bila kuongeza thamani ya ndani.

Hata hivyo, wachambuzi wengi wanaamini Tanzania ina nafasi ya kujijengea hadhi mpya katika uchumi wa dunia kutokana na mchanganyiko wake wa madini muhimu kama kinywe, nikeli, madini adimu ya ardhini, helium na madini mengine ya kimkakati.

Mafanikio ya diplomasia ya madini hayatapimwa kwa idadi ya mikataba au ukubwa wa uwekezaji pekee, bali kwa uwezo wa kubadilisha rasilimali hizo kuwa viwanda, ajira zenye ujuzi, teknolojia na mapato yanayowanufaisha wananchi kwa upana zaidi.

Jua linapotua juu ya vilima vya Mahenge, tingatinga zinaendelea kusafisha maeneo ya mradi, huku Tanzania ikiendelea kujenga nafasi yake katika ushindani wa kimataifa wa madini muhimu ya kimkakati.

Katika enzi ya nishati safi na teknolojia za kisasa, utajiri wa taifa hautapimwa tu kwa kilicho chini ya ardhi, bali kwa kile kinachojengwa juu yake kupitia diplomasia, uwekezaji na uwezo wa kugeuza rasilimali kuwa maendeleo ya kweli kwa wananchi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button