Tanzania nafasi ya pili Afrika ubora mazao ya nyuki

TABORA: TANZANIA imeshika nafasi ya pili barani Afrika kwa ubora wa mazao ya nyuki hususani asali iliposhiriki maonesho yaliyofanyika Afrika Kusini 2025.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, Dk John Mboya amesema hayo kwenye Maadhimisho ya Siku ya Nyuki Duniani viwanja vya kumbukumbu ya Vita mkoani Tabora .

Dk Mboya amesema licha kushika nafasi ya pili  Afrika, Mkoa wa Tabora ni mchangiaji mkubwa wa mazao hayo ikiwa imashika nafasi ya kwanza hapa nchini.

“Tanzania tulipoenda kwenye maonyesho ya Asali Afrika Kusini mwaka jana tulichukua nafasi ya pili,”amesema Dk Mboya.

Dk Mboya amesema uzalishaji wa asali kwa mwaka jana ulifikia watani wa tani 33 000, nchi nzima na mkoa wa Tabora uliweza kuzaisha wastani tani 16,000  za asali sawa na nusu ya uzalishaji wote nchini.

“Inasemekana asali ya Tabora inaongoza kwa vile tunayo misitu mingi na nyuki wanapenda misitu kwenye ikolojia ,mazingira mazuri na hali ya hewa kuliko sehemu yoyote Tanzania,” amesema Dk Mboya.

Dk Mboya amesema mkakati wa mkoa huo kwa sasa ni kuongeza mnyororo wa thamani kwa kile kinachozalishwa na kuuza  ili wafugaji anufaike zaidi na mazao ya nyuki.

“Dhana ya kuongeza thamani itatusaidia na kufanya  Tabora kwa miaka ijayo uwe ni mzalishaji wa bidhaa za mazao ya nyiki zenye ubora wa hali ya juu zinazoweza zikapenya kwenye masoko mbalimbali ya kimataifa,”amesema Dk Mboya.

Dk Mboya amesema katika uimarishaji uzalishaji ni muhimu kuendelea kuzingatia tafiti  zinazotolewa na Taasisi za Utafiti kwa Serikali kuzitumia   ili kuwasaidia wakulima hasa wafugaji wa nyuki  waweze kuboresha mazao ya nyuki.

Kwa upande wake Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS),Hussein Msuya, amesema kumekuwepo na maendeleo makubwa kwenye sekta ufugaji wa nyuki nchini.

Msuya ambaye pia ni Meneja wa Rasilimali za Nyuki TFS  amesema makundi makubwa ya wanawake  na vijana wamejitiokeza kuwa ni wazalishaji wa mazao ya nyuki hususani asali na kujipatia kipato.

Amesema hatua hiyo imechangiwa kwa kiwango kikubwa na  matumizi ya mizinga ya kisasa tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma ikitumika mizinga ya asili.

Msuya amesema Wakala huo unaendelea kutoa msisitizo kila mtu apate elimu ya uhifadhi kwa sababu changamoto kubwa nyuki ambao ni viumbe wanahitaji kutunzwa katika mazingira yao.

Amesema  elimu ya uhifadhi sio kuzalisha asali pekee yake bali ni uhifadhi wa kuhakikisha kwamba ile miti ya asili ambayo inatoa asali inaendelea kuwepo kwa manufaa ya uzalishaji wa mazao ya nyuki na manufaa kwa chakula.

Msuya amesema nyuki wanakabiliwa na changamoto kwenye matumizi ya kemikali katika kilimo, uharibifu wa mazingira ,uchomaji wa moto  na mabadiliko ya tabianchi vyote hivyo vinasababisha nyuki wapate mazingira magumu ya kufanya kazi.

“Elimu tunazozitoa zinatakiwa ziendane na uzalishaji, uhifadhi wa mazingira na matumizi ya teknolojia katika uzalishaji wa asali,”amesema Msuya.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button