Mgahawa wa Kijapani unavyonogesha utalii Zanzibar

Zanzibar. Sekta ya ukarimu na utalii visiwani Zanzibar imepata msukumo mkubwa wa mtindo wa maisha baada ya uliojikita kuandaa na kuuza vyakula vya asili ya Kijapani wa Maru Restaurant kuanza kutoa huduma hiyo katika eneo jipya la Africa House Garden, Stone Town.
Mgahawa huo unaleta vyakula halisi vya Kijapani katika soko la upishi na utalii linalokua kwa kasi Zanzibar. Menyu yake inajumuisha, sushi, sashimi na aina mbalimbali za vitafunwa vya kitamaduni vya Kijapani, vilivyolenga watalii wa kimataifa pamoja na wakazi wa ndani wanaotafuta huduma bora za ulaji.
Ikiwa kwenye ukingo wa maji wa Stone Town, Africa House Garden, imekuwa haraka miongoni mwa maeneo mapya ya starehe na mtindo wa maisha Zanzibar, kwa kuchanganya migahawa, burudani na maeneo ya starehe kwa umma yanayoelekea Bahari ya Hindi.
Mradi huu ni moja ya miradi iliyokamilishwa na kutekelezwa na Infinity Developments, Kampuni ya ukarimu na mali isiyohamishika kutoka Dubai, inayojulikana kwa miradi mingi ya utalii na ukarabati wa miji kote Zanzibar.
Wadau wa sekta ya ukarimu wanasema ufunguzi huu unaonyesha jinsi tasnia ya utalii ya Zanzibar inavyobadilika, huku wageni sasa wakitafuta zaidi uzoefu unaohusisha mtindo wa maisha, unaozidi kuvuka utalii wa pwani wa kawaida.
“Soko la utalii linabadilika kwa kasi. Wageni leo wanataka uzoefu mbalimbali — kuanzia afya, utamaduni, hadi vyakula vya kimataifa na burudani za ukingo wa maji,” alisema mdau mmoja wa utalii Stone Town.
Mbali na kupanua aina za vyakula vinavyopatikana Zanzibar, mradi huu pia unatoa fursa za ajira kwa wakazi wa eneo hilo. Mgahawa na maeneo yanayouzunguka wameajiri wafanyakazi wengi wa Kizanzibari katika idara za ukarimu, huduma za vyakula na uendeshaji.
Wataalamu wa sekta wanasema uwekezaji wa namna hii unazidi kuwa muhimu kuhakikisha ukuaji wa utalii unaleta manufaa mapana kiuchumi na kuongeza ujuzi kwa jamii za wenyeji.
Ufunguzi huu pia unaangazia ongezeko la uwekezaji wa sekta binafsi katika miundombinu ya utalii na mtindo wa maisha Zanzibar, hususan Stone Town, ambako wawekezaji sasa wanajumuisha ukarimu, biashara ya rejareja na maeneo ya starehe ndani ya miradi mchanganyiko ya ukingo wa maji.

Africa House Garden, yenyewe imekuwa nyongeza kubwa katika taswira ya ukarimu wa Stone Town, ikiwavutia wakazi na watalii kupitia eneo lake la ukingo wa bahari, maeneo ya burudani na dhana mbalimbali za ulaji.
Maendeleo haya yanakuja wakati ujenzi wa daraja jipya la majini linalopakana na bustani hiyo unaendelea, mradi unaotarajiwa kuboresha upatikanaji kupitia baharini na kuunga mkono safari za utalii, boti za starehe na shughuli za ukingo wa maji.
Wachambuzi wanasema uwekezaji katika miundombinu jumuishi ya mtindo wa maisha unazidi kuwa muhimu kadri Zanzibar inavyoshindana na maeneo mengine ya Bahari ya Hindi katika kuvutia utalii wa thamani kubwa na uwekezaji wa kimataifa wa ukarimu.
Infinity Developments, imekuwa ikiimarisha uwepo wake Zanzibar katika miaka ya hivi karibuni kupitia miradi ya ukarimu, ukarabati wa urithi na miradi mchanganyiko inayolenga kuunga mkono uchumi wa utalii unaokua wa visiwa hivyo.
Kampuni hiyo kwa sasa inahusika katika miradi kadhaa mikubwa, ikiwemo; Anantara Zanzibar Resort & Residences, NH Collection Pemba Wellness Resort, Infinity Hills, na miradi ya ukarabati ndani ya Stone Town.
Kadri idadi ya watalii wa kimataifa inavyoendelea kuongezeka na maslahi ya wawekezaji yakipanda, wadau wanaamini miradi kama Africa House Garden na Maru Restaurant, itasaidia zaidi kubadilisha mseto wa utalii wa Zanzibar, huku ikiweka Stone Town katika nafasi ya kuwa kitovu kipya cha mtindo wa maisha na upishi ndani ya eneo la Bahari ya Hindi.



