Spika Zungu aifunda Wizara ya Ujenzi

DAR ES SALAAM: Spika wa Bunge, Mussa Azan Zungu, ameishauru Wizara ya Ujenzi kwa kuonyesha hamasa ya kuingia katika mfumo wa Ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi (PPP).
Zungu amesema bila PPP, mzigo wa ujenzi na matengenezo ya barabara ni mkubwa mno kwa serikali peke yake.
Alieleza kuwa katika mataifa mengi duniani, serikali huingia ubia na sekta binafsi ili kugawana gharama na majukumu ya miundombinu. “Barabara hulipiwa Ushuru na watumiaji na hivyo serikali hupunguza mzigo wa kifedha,” alisema.
Kwa mujibu wa Spika, mahitaji ya barabara na miundombinu nchini bado ni makubwa mno huku akisisitiza kuwa ni wakati muafaka Wizara ya Ujenzi kuonyesha hamasa ya kweli hasa katika kutekeleza Mpango wa Nne wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano(FYDPIV 206/27-2030/31) ambapo asilimia 70 ya miradi ya maendeleo imepangwa kutekelezwa na sekta binafsi.
Hata hivyo, alionyesha masikitiko kwamba Wizara bado inang’ang’ania kufanya kila kitu yenyewe, bila kuona faida kubwa ya kushirikiana na sekta binafsi. “Je, ni faida gani hasa mnayopata kwa kuendelea kubeba mzigo huu peke yenu?” alihoji Spika Zungu kwa ukali.
Aidha, alikumbusha kuwa mataifa mengine yalianza kuingia kwenye PPP miaka ishirini iliyopita na sasa wanavuna matunda ya ushirikiano huo. “Sisi pia tunapaswa kuanza safari ya ubia huu sasa, ili tusiachwe nyuma katika mbio za maendeleo,” aliongeza.
Kauli ya Spika Zungu ni wito kwa Wizara ya Ujenzi kuacha kusita na kuanza kushirikiana na sekta binafsi. Hii inaonesha kuwa PPP si chaguo tena, bali ni hitaji la msingi ili kufanikisha malengo ya Vision 2050 na kupunguza mzigo wa kifedha kwa taifa na hivyo kuwaletea Wananchi nafuu ya maisha.



