Kiswaga atoa mifuko 120 ya simenti ujenzi kituo cha afya Masaka

IRINGA: Mbunge wa Jimbo la Kalenga, Jackson Kiswaga ameendelea kuunga mkono maendeleo ya wananchi baada ya kukabidhi mifuko 120 ya saruji kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa Kituo cha Afya katika Kata ya Masaka jimboni humo.
Hatua hiyo imekuja baada ya hivikaribuni kukabidhi msaada wa mifuko 200 ya simenti katika Shule ya Sekondari Tosamaganga kwa ajili ya ujenzi wa kiwanja cha mpira wa kikapu.

Pamoja na msaada huo, mbunge huyo alijibu baadhi ya kero zilizowasilishwa na wananchi kupitia Diwani wa Kata ya Masaka, Yohanes Sanga, zikiwemo changamoto za umeme, maji, barabara, afya na kilimo cha umwagiliaji.
Akishukuru kwa msaada huo, Sanga alisema kwa sasa Kata ya Masaka haina kituo cha afya wala zahanati, hali inayowalazimu wananchi kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za matibabu.
Alisema mpango wa awali ulikuwa kuanza ujenzi wa zahanati katika kila kijiji, lakini kwa lengo la kuharakisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi wa kata nzima, viongozi wamekubaliana kuanza na ujenzi wa Kituo cha Afya kitakachohudumia vijiji vya Makota, Sadani na Kaning’ombe.

“Kwa niaba ya wananchi wa kata hii, nikushukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa msaada huu ambao utatusaidia kufungua njia ya kuanza ujenzi wa kituo hicho,” alisema Sanga.
Hata hivyo, alisema ujenzi wa kituo hicho utaanza baada ya wataalamu kutoa ushauri wa eneo sahihi litakalofaa kujengwa.
Akizungumzia changamoto nyingine za kata hiyo, Diwani Sanga alisema licha ya baadhi ya maeneo kupata huduma ya umeme kupitia REA, bado kuna vitongoji ambavyo havijafikiwa na huduma hiyo.
Katika sekta ya kilimo, alisema wananchi wanahitaji mradi wa umwagiliaji kupitia Mto Lupalama ili bwawa lililopo liweze kuwa na manufaa kwa wakulima wa kata nzima.
“Kata yetu ina wakulima wengi wenye uwezo mkubwa na shauku ya kufanya kilimo cha umwagiliaji. Tunaomba utusaidie kufikisha ujumbe wetu serikalini ili jambo hili lifanyiwe kazi,” alisema Sanga.
Wananchi pia walilalamikia ubovu wa barabara ya Tanangozi kuelekea Masungati na Mseke, uhaba wa walimu pamoja na uchakavu wa majengo ya Shule ya Sekondari Mseke.
Akizungumza mbele ya wananchi, Kiswaga alisema serikali itaendelea kushughulikia changamoto hizo kwa kuzingatia mapato na vipaumbele vya maendeleo.
“Sera ya serikali ni kuhakikisha kila kata inakuwa na kituo cha afya na kila kijiji kinapata zahanati. Nimeleta mifuko 120 ya saruji na nitaendelea kuchangia hatua kwa hatua hadi mradi ukamilike,” alisema Kiswaga.
Kuhusu umeme, alisema serikali itaendelea kupeleka huduma hiyo katika vitongoji vilivyobaki na kwamba ifikapo mwaka 2030 changamoto kubwa ya umeme vijijini itakuwa imepungua kwa kiasi kikubwa.
Mbunge huyo pia aliwataka wananchi kutouza ardhi ovyo, akisema migogoro mingi ya ardhi husababishwa na ukiukwaji wa taratibu katika ngazi za vijiji.



