SUA kutekeleza miradi ya utafiti ya Sh bilioni 3.4

MOROGORO: CHUO Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimeanza utekelezaji wa miradi mipya 12 ya utafiti yenye jumla ya thamani ya Sh bilioni 3.4.
Miradi hiyo ni yenye lengo la kukuza maarifa na kutatua changamoto kwenye sekta ya kilimo, mifugo, mazingira na maendeleo ya jamii kwa ujumla.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu hicho, Profesa Raphael Chibunda amesema hayo kwenye mahafali ya 47 ya ambapo jumla ya wahitumi 877 walitunukiwa shahada mbalimbali na Mkuu wa Chuo na Waziri Mkuu Mstaafu Jaji Joseph Warioba.

Profesa Chibunda amesema kuanza kwa miradi hiyo kumekifanya chuo kufikisha jumla ya miradi ya utafiti 130 ambayo inaendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini.
Chuo kinaendelea kuhimiza matumizi ya matokeo ya tafiti zetu katika kuchangia sera na mipango ya taifa, na katika kipindi hiki cha taarifa tumeanza utekelezaji wa miradi mipya yenye thamani ya Sh bilioni 3.4″ amesema Profesa Chibunda.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Chuo kikuu hicho, Andrew Masawe amesema Baraza limeendelea kupokea taarifa za utekelezaji wa miradi mbalimbali ambapo kiasi cha Sh bilioni 59.6 zimetengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Masawe amesema chuo kimeendelea kuhimiza utengenezaji na ukarabati wa miundombinu ya chuo kupitia mapato ya ndani jambo ambalo limetekelezwa kwa ufanisi mkubwa na miradi ya ukarabati ikiendelea vizuri.
Amesema pia Baraza linaen kusimamia matumizi bora ya fedha na ufatiliaji wa utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026.
Nao baadhi ya wahitimu akiwemo Calvin Gwabara ambaye ni mhitimu wa shahada ya Umahili wa Habari na Menejimenti ya Maarifa ya Chuo hicho amesema kuwa tafiti zinazofanywa na wataalam kutoka SUA zimekuwa zikileta tija ya moja kwa moja kwa wananchi wa kawaida.
Gwabara amesema katika utafiti alioufanya alibainisha umuhimu wa matumizi ya vyombo vya habari katika kuchangia ukuazaji na uongezaji wa mavuno kwa wakulima hasa kupitia vipindi vya kilimo vilivyokuwa vikirushwa na kituo cha redio cha chuo hicho SUA FM.
“Ni kweli kuna umuhimu mkubwa wa Serikali na jamii kutumia matokeo ya utafiti unaofanywa na watafiti, hasa tafiti hizi zikiwafikia wakulima moja kwa moja” amesema Gwabara.
Amesema matokeo ya matunda ya tafiti hizo huonekana kwa wakulima kwa muda mfupi kupitia mavuno yao kama mkulima alikuwa anavuna gunia 10 kwa ekari moja na hivyo kuwesha mavuno yake hupanda hadi kufikia gunia 30 hadi 40 kwa ekari.



