Watano washtakiwa usafirishaji wa madawa ya kulevya

WATU watano wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashitaka mawili ya kusafirisha madawa ya kulevya aina ya Heroin gramu 5309.57 na Cocaine gramu 894.28 yenye thamani ya Shilingi 328,078,100.

Washitakiwa hao ni Muharami Abdallah (Chonji), Abdul Chumbi, Rehani Umande,Tanaka Mwakasagule na Maliki Maunda wote ni wakazi wa Dar es Salaam. Walisomewa mashitaka hayo Jana na Wakili wa Serikali, Yusuph Aboud akisaidiana na Tumaini Mafuru mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu,Mary Mrio.

Akisoma hati ya mashitaka, wakili Abood alidai katika shitaka la kwanza la kusafirisha madawa ya kulevya washitakiwa wote mnamo Octoba 21, 2014 katika eneo la Magomeni Makanya walisafirisha gramu 5309.57 za dawa aina ya Heroin Hydrochloride yenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 265.

Katika shtaka la pili alidai washitakiwa wote wakiwa Magomeni walisafirisha gramu 894.28 za dawa aina ya Cocaine Hydrochloride yenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 62. Aboud aliieleza mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika.
Mrio alisema washitakiwa hawaruhusiwi kujibu chochote kwakuwa mahakama haina Mamlaka ya kusikiliza shitaka hilo. Washitakiwa hao wamerudishwa mahabusu hadi Desemba 21, mwaka huu ambapo kesi hiyo itakuja kwa ajili ya kutajwa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button