Watu 1,066 wamepoteza maisha ajali 2025/26

DODOMA; SERIKALI imesema watu 1,066 walipoteza maisha kutokana na matukio ya ajali za barabarani kuanzia Julai 2025 hadi Aprili 2026, ikilinganishwa vifo 1, 275 vilivyotokea kipindi kama hicho mwaka 2024/25.

Kauli hiyo imetolewa bungeni na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya wizara hiyo kwa mwaka 2026/27.

“Takwimu zinaonesha kuwa, matukio ya usalama barabarani yaliyotolewa taarifa katika vituo vya polisi nchini yamepungua kutoka 1,322 katika kipindi cha Julai 2024 hadi Aprili 2025 na kufikia 1,233 katika kipindi kama hicho kwa mwaka 2025/26.

“Katika matukio hayo, jumla ya watu 1,066 walipoteza maisha ikilinganishwa na watu 1,275 waliopoteza maisha katika kipindi kama hicho kwa mwaka 2024/25 ikiwa ni upungufu wa asilimia 16.4.

“Vilevile, watu 1,869 walijeruhiwa ikilinganishwa na watu 2,278 waliojeruhiwa kwa kipindi kama hicho mwaka 2024/25 ikiwa ni upungufu wa asilimia 18. 42.

“Katika mwaka 2026/27 wizara kupitia Jeshi la Polisi itaendelea na mikakati ya kusimamia ipasavyo sheria ya usalama barabarani kwa kufanya doria na kuchukua hatua stahiki kwa wanaokiuka sheria hiyo.

“Pia, wizara kupitia jeshi itaendelea kushirikiana na wadau wengine kutoa elimu kwa umma kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kuhusu matumizi sahihi ya barabara kwa mujibu wa sheria. Hatua hizo zinalenga kuimarisha hali ya usalama barabarani,” amesema Waziri Katambi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button