Wabunge walia uvamizi maeneo ya wazi, michezo

DODOMA; Wabunge wameishauri serikali kuweka mikakati ya kurejesha maeneo yote ya wazi yaliyovamiwa na kuhakikisha kuwa inasimamia kikamilifu utengaji na utunzaji wa maeneo ya wazi nchini.

Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya makazi kwa Mwaka wa Fedha 2025/26, pamoja na maoni ya kamati kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya wizara kwa kwa mwaka wa fedha 2026/27, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mary Masanja  amesema maeneo hayo hayapaswi kubadilishwa matumizi bila idhini ya wizara.

“Utengaji na usimamizi wa maeneo ya wazi nchini unaongozwa na Sheria ya Mipango Miji, Sura 355 (Urban Planning Act, Cap 355).

“Sheria hii inazipa mamlaka za upangaji jukumu la kutenga, kupima, kutunza na kulinda maeneo ya wazi chini ya usimamizi wa Wizara ya Ardhi.

“Maeneo yote ya wazi kama vile viwanja vya michezo, bustani na maeneo ya kupumzikia ni mali ya umma na hayapaswi kubadilishiwa matumizi bila idhini maalumu ya wizara.

“Mheshimiwa Spika, kwa sasa maeneo mengi ya wazi ni vigumu kuyatambua kutokana na uvamizi unaofanywa na wananchi kwa kushirikiana na watumishi wa wizara ambao huuziana kinyemela na kubadili matumizi.  Vilevile baadhi ya mitaa haijatengewa kabisa maeneo hayo.

“Kamati inaishauri serikali kuweka mikakati ya kurejesha maeneo yote ya wazi yaliyovamiwa na kuhakikisha kuwa inasimamia kikamilifu utengaji na utunzaji wa maeneo ya wazi nchini,” amesema Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button