Wanne wafa, 29 wajeruhiwa ajali ya basi Mbeya

MBEYA: Watu wanne wamefariki na wengine 29 kujeruhiwa kufuatia ajali ya basi la abiria iliyotokea mkoani Mbeya baada ya gari hilo kuacha njia na kupinduka katika eneo lenye kona kali kwenye barabara ya Mbeya kuelekea wilayani Chunya.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga, amesema ajali hiyo ilitokea Mei 31, 2026, majira ya saa tisa alasiri katika eneo la Maji Mazuri, kando ya barabara ya Mbeya–Chunya.

Kwa mujibu wa Kamanda Kuzaga, ajali hiyo ilihusisha basi la abiria la Kampuni ya Mwasote lenye namba za usajili T134 DFB, aina ya Mitsubishi, lililokuwa likitoka Mbeya kuelekea Chunya.

Basi hilo lilikuwa likiendeshwa na dereva Nehemia Sanga (50), mkazi wa Uyole, ambaye alishindwa kulimudu gari katika eneo lenye kona kali, hivyo kuacha njia na kupinduka.

Amesema watu waliofariki katika ajali hiyo ni wanaume watatu na mwanamke mmoja anayekadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 35 na 40,Kati ya marehemu hao, wawili wametambuliwa kuwa ni Hamza (30) na Matrida Mwabanganya anayekadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 30 na 36.

Aidha, watu 29 walijeruhiwa katika ajali hiyo, wakiwemo wanaume 24 na wanawake watano,Kati ya majeruhi hao, 11 wamelazwa hospitalini kwa matibabu, huku 18 wakitibiwa na kuruhusiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya.

Kamanda Kuzaga amesema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva kushindwa kulimudu gari katika eneo lenye kona kali, hali iliyosababisha basi hilo kuacha njia na kupinduka.

Ajali hiyo imetokea ikiwa ni siku moja tu tangu kutokee ajali nyingine mkoani Mbeya iliyosababisha vifo vya watu watatu. Ajali hiyo ilihusisha basi la abiria la Kampuni ya ABC Upper Class kugongana uso kwa uso na lori katika Kijiji cha Mambi, Wilaya ya Mbarali.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button