Hanang yafikia 97% upatikanaji maji

MANYARA: Upatikanaji wa Maji katika Wilaya ya Hanang’ mkoani Manyara sasa umefikia asilimia 97, huku zaidi ya wananchi 35,000 wilayani humo wanatajwa kunufaika na huduma ya maji kupitia mradi Mradi wa Chujio la Maji la Jorodom wenye thamani ya Sh bilioni 1.1.
Akizungumza mara baada ya kukagua mradi huo leo Juni Mosi, 2026 Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Kenani Kihongosi, amesema mradi huo ni ushahidi na kielelezo cha utekelezaji wa kaulimbiu ya CCM ya ‘Kazi na Utu’.

Kihongosi amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan inavyoendelea kutatua changamoto zinazowagusa wananchi moja kwa moja.
“Kazi kubwa inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita inaonekana wazi kwa wananchi. Huu ni mfano wa namna ahadi zinavyotekelezwa kwa vitendo kwa kuwapelekea wananchi huduma muhimu zinazoboresha maisha yao ya kila siku,” amesema Kihongosi.
Amesema upatikanaji wa maji safi na salama ni miongoni mwa mahitaji muhimu ya wananchi na kwamba kukamilika kwa mradi huo kumeondoa adha iliyokuwa ikiwakabili maelfu ya wakazi wa Hanang’ kwa miaka mingi.

Aidha, amesema mafanikio ya mradi huo yametokana na usimamizi mzuri wa Serikali pamoja na viongozi wa CCM katika kufuatilia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi, jambo lililowezesha mradi kukamilika kwa wakati na kuanza kutoa huduma kwa wananchi.
Katika hatua nyingine, Kihongosi amekumbusha namna serikali ilivyowasimamia wananchi wa Hanang’ wakati wa maafa ya maporomoko ya matope na mawe yaliyosababisha madhara makubwa kwa wakazi wa eneo hilo.
Amesema hatua zilizochukuliwa na serikali ikiwemo ujenzi wa nyumba za waathirika na urejeshaji wa miundombinu muhimu, zinaonesha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wanapata msaada wakati wa changamoto na huduma bora wakati wa maendeleo.

Awali akitoa taarifa ya mradi huo, Mkurugenzi Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Babati (BAWASA), Iddi Msuya amesema mradi huo ulioanza mwaka 2022 na kukamilika mwaka 2025 umeongeza upatikanaji wa maji katika wilaya hiyo hadi kufikia asilimia 97 na una uwezo wa kuzalisha zaidi ya lita milioni 2.5 za maji kwa siku.
Amesema Mradi huo unagharimu zaidi ya Sh bilioni 1.1 katika utekelezaji wake na unahudumia zaidi ya wananchi 35,000.
Ameongeza kuwa wanaendelea na uchimbaji wa visima vitatu ambavyo kukamilika kwake kutafanikisha kufikia uzallishaji wa maji zaidi ya lita milioni sita.



