Dk Nguvila asisitiza ushirikiano wa kisekta Arusha

ARUSHA: Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha Dk, Toba Nguvila, amewasisitiza watendaji wa serikali katika mkoa huo, kuanzia sekretarieti ya mkoa, halmashauri taasisi na mashirika yote ya umma, kufanya kazi kwa ushirikiano kisekta ili kutimiza adhma ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na kwa wakati.
Dk Nguvila ametoa rai hiyo wakati akifungua kikao kazi cha robo ya mwisho kilichowakutanisha watendaji wa serikali wa mkoa huo kutathmini utendaji wa shughuli wa serikali kwa mwaka wa fedha 2025/2026.

“Lengo la kikao kazi hiki ni kutathmini utendaji wa shughuli za serikali kwa Mkoa, kuona mafanikio na kubaini changamoto zilizojitokeza, utakaotoa dira na mwelekeo wa utekelezaji wa shughuli za Serikali kwa mwaka mpya wa fedha wa 2026/27, kukiwa na mipango thabiti na mwelekeo wa utekelezaji, kukiwa na uelewa wa pamoja miongoni mwa watalamu wote,”amesema.

Aidha, Dk Nguvila ameweka wazi kuwa, kikao hicho kitatumika kama sehemu ya kufahamiana na kutatua migongano na migogoro mbalimbali miongoni mwa washiriki wa Kikao hicho pamoja na kushughulikia kwa pamoja sintofahamu zilizopo baina ya halmashauri, sekretarieti ya mkoa pamoja na taasisi za umma zilizopo katika Mkoa wa Arusha.



