Wanafunzi Shinyanga wanufaika huduma vyoo bora

SHINYANGA: ZAIDI ya wanafunzi 600 wa shule za msingi katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga wamenufaika na huduma ya miundombinu ya mazingira baada ya Shirika la Water for Good kujenga vyoo 22 vyenye matundu 93.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi kutoka Shirika la Water for Good nchini Tanzania Devocatus Kamara katika hafla ya makabidhiano ya miundombinu ya matundu ya vyoo 15 na machoteo ya maji 12 katika Shule ya Msingi Masekelo iliyopo kata ya Bukene Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga.

Kamara amesema walianza utekelezaji wa miundombinu hiyo kwaajili ya kuboresha huduma ya elimu na mazingira kwenye Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga kuanzia mwaka 2021 hadi sasa nakufanikiwa kutekeleza adhima hiyo kwa wananchi.
“Makabidhiano ya leo yanaonyesha uwajibikaji wa pamoja nani sehemu ya kuboresha huduma bora kwa jamii ikiwa ushirika huu ni kutoka shirika hilo kwa kuboresha mazingira kwa kuchochea elimu”amesema Kamara.
Mhandisi kutoka shirika la Water for Good aliyekuwa msimamizi wa mradi huo Raphael Lwassa amesema walianza mwezi Novemba 2025 ujenzi wa Matundu ya vyoo 15, koki 12 za kuchotea maji na Matundu ya Vyoo Zahanati ya Simbigu uliogharimu zaidi ya Sh milioni 56.

“Wakala wa Maji safi na Mazingira vijijini (Ruwasa) imekuwa ikitekeleza mradi wa maji kwenye vijiji vitatu vya Sumbigu Masekelo na Bukene kwa kuweka ghati lakini sisi Water for Good tumeweka koki kwa gharama ya shilingi Milioni 4.8,Matundu ya vyoo shule ya msingi Masekelo kwa shilingi Milioni 32.5 na Matundu ya vyoo matano kwenye Zahanati ya kijiji cha Simbigu kwa Sh milioni 18,”amesema Mhandisi Lwassa.
Mhandisi Lwassa amesema upande wa miundombinu ya matundu ya vyoo wanafunzi 223 wa kike watatumia matundu ya vyoo nane ikiwa chumba kimoja nicha kujisriri na wavulana 211 matundu saba huku wakifuata muongozo wa serikali wa utumiaji Wash na kuwajali watu wenye ulemavu.

Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga, Hamduni Salum ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye makabidhiano hayo alisema mradi huo ambao uko tayari utakwenda kuwahudumia wanafunzi kwa matumizi ya kutoa huduma safi na kuboresha mazingira mazuri ya kujifunzia.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga ambaye ni Ofisa Elimu Msingi Andrew Mitumba amesema mradi huu kwenye shule ya masekelo utathibiti utoro na utaongeza ufaulu kwani wanafunzi waliokuwa wakihangaika zaidi na wakati mwingine kupoteza masomo na jamii ione na ijifunze ujenzi wa vyoo kama hivi.



