TAMONGSCO yatoa neno kodi za mitaa

ARUSHA: Shirikisho la Wamiliki na Mameneja wa Shule na Vyuo Visivyo vya Serikali Tanzania (TAMONGSCO) wamezitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa kuacha kutoza kodi na tozo ambazo tayari zilisamehewa na Serikali Kuu, wakidai kuwa baadhi ya halmashauri zinatumia nguvu na askari mgambo kukusanya fedha hizo kinyume na sheria.

Malalamiko hayo yameelekezwa zaidi kwa Halmashauri ya Jiji la Arusha na Halmashauri ya Arusha Vijijini, ambazo zinadaiwa kuendelea kukusanya kodi zisizotambulika na Serikali Kuu, jambo linalosababisha sintofahamu na kuathiri utoaji wa huduma za elimu.

Wakizungumza na waandishi wa habari Jijini Arusha, viongozi wa Shirikisho la Wamiliki na Mameneja wa Shule na Vyuo Visivyo vya Serikali Tanzania (TAMONGSCO) walisema shule binafsi zinakabiliwa na zaidi ya tozo na kodi 11, zikiwemo ushuru wa huduma (Service Levy), ada za mitihani, leseni za mabango ya shule pamoja na michango mbalimbali ya michezo.

Mtendaji Mkuu wa TAMONGSCO, Benjamin Nkonya, amesema baadhi ya tozo zinazodaiwa na halmashauri hizo ni kinyume na maelekezo ya Serikali Kuu na zinawaongezea mzigo wamiliki wa shule binafsi.

Amesema pamoja na ushuru wa huduma, shule hizo pia zinadaiwa fedha za uchapishaji wa mitihani na michango ya mashindano ya michezo na Taaluma kwa shule za Msingi za Tanzania kwa shule za Msingi Tanzania(UMITASHUMTA a Umoja wa Michezo kwa Shule binafsi za Sekondari Tanzania (UMISETA), ambazo kwa mujibu wao hazina manufaa ya moja kwa moja kwa taasisi hizo.

“Tunachohoji ni matumizi ya nguvu katika ukusanyaji wa kodi, inakuwaje mgambo wenye silaha wanaingia shuleni kudai kodi au kufunga shule? Sisi tunaipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kukaa na walipakodi na kutoa elimu kisha kutoa muda wa mhusika kulipa kodi na halmashauri nazo zinapaswa kufuata utaratibu huo badala ya kutumia nguvu, lakini iweje zikisanye kodi zilizofutwa na serikali kwa sheria ipi? alisema Nkonya.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TAMONGSCO Kanda ya Kaskazini, Leonard Mao, amesema kumekuwa na malalamiko ya muda mrefu kuhusu utozwaji wa kodi hizo, lakini juhudi zao za kutafuta ufafanuzi kutoka kwa mamlaka husika bado hazijazaa matunda.

“Tunaomba serikali itoe mwongozo wa wazi kuhusu kodi zinazopaswa kulipwa na shule binafsi,halmashauri zisitumie mabavu kukusanya fedha ambazo zilisamehewa kisheria.,walimu na wamiliki wa shule wanadhalilishwa mbele ya wanafunzi kwa kufuatwa na mgambo wenye silaha,”

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button