Abuni mashine kuokoa watoto njiti

ARUSHA: Mbunifu Mosety Baita kutoka jijini Arusha amebuni mashine maalumu ya kisasa inayolenga kuokoa maisha ya watoto wanaozaliwa kabla ya muda wao (njiti), pamoja na kusaidia huduma za afya kwa mama wajawazito na watoto wachanga.

Baita ameonyesha mashine hiyo mbele ya Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa wakati akikagua mabanda ya maonesho kabla ya ufunguzi wa Kongamano Kuu la Mwaka la 33 la Taasisi ya Taifa ya Utafiti  wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) linalofanyika Arusha kuanzia leo Juni 9-12.

Amesema mashine hiyo imeundwa kwa teknolojia ya kipekee inayowezesha huduma mbalimbali kufanyika katika kifaa kimoja, tofauti na vifaa vingine vinavyohitaji mtoto kuhamishwa kutoka sehemu moja kwenda nyingine kwa ajili ya vipimo na matibabu.

Amesema katika hospitali nyingi, ikiwemo baadhi ya hospitali za rufaa, watoto wanaozaliwa kabla ya muda hulazimika kupelekwa katika vitengo tofauti kwa ajili ya vipimo mbalimbali kutokana na ukosefu wa vifaa vinavyoweza kutoa huduma zote kwa pamoja.

“Teknolojia hii imekuja kutatua changamoto hiyo kwa kuwezesha uchunguzi na huduma mbalimbali kufanyika katika eneo moja bila kumhamisha mtoto, jambo ambalo hupunguza hatari na kuongeza nafasi ya kuishi kwa watoto njiti,”

Mbunifu huyo ameeleza kuwa uvumbuzi huo tayari umepata hati miliki (Patent Rights), hatua inayothibitisha umiliki wa kisheria wa teknolojia hiyo na kuipa ulinzi dhidi ya matumizi yasiyoidhinishwa.

Ambapo Waziri Mchengerwa amesisitiza wizara ya Afya itakuwa bega kwa bega na mbunifu huyo kwani  kupata hati miliki ni mafanikio makubwa kwa wabunifu wa ndani na kunafungua fursa za matumizi mapana ya teknolojia hiyo katika hospitali za Tanzania na nje ya nchi.

“Lengo letu ni kuona watoto wengi zaidi wanaozaliwa kabla ya muda wanaokolewa na kupata huduma bora kwa kutumia teknolojia iliyobuniwa hapa nchini,”

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button