Wataalamu kukutana Mwanza kujadili changamoto za jamii

MWANZA: WATALAAMU wa Maendeleo ya Jamii nchini wanatarajia kukutana katika mkutano mkuu wa mwaka kwa lengo la kujadili changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii ikiwemo mmomonyoko wa maadili na ukatili wa kijinisa.
Maafisa maendeleo hao zaidi ya 1,260 watakutana katika kikao cha siku tatu kuanzia Juni 17 -19 mwaka huu kwenye mkutano mkuu wa mwaka wa Chama cha Wataalam wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (CODEPATA) kitakachofanyika jijini Mwanza.
Hayo yamesemwa leo na Rais wa Chama hicho, Victor Kabuje wakati wa mkutano maalumu na waandishi wa habari jijini Mwanza. Akielezea kuhusu mkutano huo, Kabuje amesema utakawakutanisha maafisa maendeleo ya jamii kutoka taasisi mbalimbali za Serikali na sekta binafsi nchini.
Amesema mkutano una lengo la kujadili na kutafakari changamoto zinazoikabili jamii pamoja na kuweka mikakati ya maendeleo endelevu.
Amesema mkutano huo ni wa siku tatu utaanza Juni 17 mpaka Juni 19 mkoani Mwanza. Amesema mkutano huo utatoa fursa kwa wataalamu wa maendeleo ya jamii kujadili masuala mbalimbali yanayohusu ustawi wa jamii na maendeleo ya taifa.
Aliongeza kuwa mkutano huo wa kitaaluma wa mwaka utalenga kubadilishana uzoefu, kutathmini mafanikio yaliyopatikana na kujadili changamoto zinazojitokeza katika sekta ya maendeleo ya jamii ili kupata suluhisho la pamoja.



