TZ, Comoro zaunganishwa safari mpya za Royah Air

DAR ES SALAAM: Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA) umeandika hatua mpya katika sekta ya usafiri wa anga baada ya kupokea rasmi safari za ndege za kampuni ya Royal Air zinazounganisha moja kwa moja Tanzania na Comoro.

Uzinduzi wa safari hizo unatarajiwa kuimarisha usafiri wa abiria, usafirishaji wa mizigo na kukuza biashara kati ya mataifa hayo mawili jirani ambayo kwa muda mrefu yamekuwa na uhusiano wa karibu wa kiuchumi na kijamii.

Akizungumza Leo wakati wa hafla ya uzinduzi wa safari hiyo Mkurugenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere, Bertha Bankwa, alisema kuanza kwa huduma za Royal Air ni mafanikio makubwa kwa sekta ya usafiri wa anga nchini kwani kunaongeza idadi ya mashirika ya ndege yanayohudumia njia ya Tanzania na Comoro.

Amesema ndege hiyo itakuwa ikifanya safari mara nne kwa wiki, siku za Jumatatu, Jumatano, Ijumaa na Jumapili. Alibainisha kuwa safari za Ijumaa zitakuwa na utaratibu maalum ambapo ndege itawasili ikiwa na abiria na kurejea Comoro ikiwa imebeba mizigo.

Bankwa amesema ujio wa Royal Air utaongeza ushindani chanya katika soko la usafiri wa anga na kusaidia kuongeza mapato ya kiwanja kupitia ongezeko la idadi ya abiria na mizigo inayosafirishwa.

Ameeleza kuwa tayari njia hiyo inahudumiwa na mashirika mengine ya ndege, yakiwemo Air Tanzania na Precision Air, jambo linaloonyesha kuwepo kwa mahitaji makubwa ya usafiri kati ya Tanzania na Comoro.

Kwa mujibu wa Bankwa, Comoro imeendelea kuwa miongoni mwa washirika muhimu wa kibiashara wa Tanzania, huku wafanyabiashara wengi kutoka visiwa hivyo wakitegemea soko la Kariakoo jijini Dar es Salaam kwa ajili ya ununuzi wa bidhaa mbalimbali.

Amesema kupatikana kwa safari za uhakika kutarahisisha zaidi usafirishaji wa bidhaa na kuongeza kiwango cha biashara kati ya nchi hizo mbili, huku akibainisha kuwa wafanyabiashara wengi wa Comoro wamekuwa wakiondoka Tanzania wakiwa na mizigo mikubwa ya bidhaa mbalimbali.

Aidha, amesisitiza kuwa kuongezeka kwa safari hizo kunafungua fursa mpya kwa Watanzania kutembelea Comoro kwa madhumuni ya biashara, uwekezaji na utalii.
Aliwataka Watanzania kutumia fursa zilizopo nchini Comoro na kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya mataifa hayo mawili, akieleza kuwa ongezeko la mashirika ya ndege yanayohudumia njia hiyo ni ishara ya kukua kwa mahitaji ya usafiri na biashara.
Bankwa alisema matarajio ya mamlaka ya kiwanja hicho ni kuona Royal Air ikiongeza idadi ya safari zake katika siku zijazo kutoka mara nne kwa wiki hadi kufikia safari za kila siku, kadri mahitaji yatakavyoendelea kuongezeka.

Kwa Upande wake Balozi wa Commoro Nchini Ahamada Elbadaoui Mohamed Fakih amesema kuanzishwa kwa safari hizo ni ushirikiano baina ya Tanzania na Commoro ambapo itaenda kukuza Uchumi pande zote .

Kuanzishwa kwa safari za Royal Air kunatajwa kuwa hatua muhimu katika kuimarisha muunganiko wa kikanda, kurahisisha biashara na kuongeza fursa za uwekezaji kati ya Tanzania na Comoro.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button