Urejeshaji duni mikopo ya elimu,teknolojia yatajwa kuwa suluhu

“MWAKA jana nilikuwa nimepata chuo  nikaomba mkopo lakini nilivyokosa, nikashindwa kwenda chuo,” anasema Singo Mrombo (20). Anaongeza: “Ninamtegemea mama yangu ambaye ndiye mzazi pekee, lakini na yeye hana uwezo wa kunilipia ada ya chuo na baba yangu mzazi sijawahi kumuona na sijui alipo.”

Singo ambaye ni mkazi wa Mbezi, Dar es Salaam, anasema kwa sasa anajishughulisha na ufundi ili kujiingizia kipato huku akisubiri ufunguzi wa dirisha jipya la mikopo ya elimu ya juu. “Sijakata tamaa, bado naamini kuwa nitapata wakati ujao na nitatimiza ndoto yangu ya kupata elimu ya chuo kikuu na kuwa daktari,” anasisitiza.

Singo ni miongoni mwa vijana waliokosa mikopo ya elimu ya juu hali iliyoathiri kutimia kwa ndoto zake za kielimu kutokana na sababu mbalimbali. Miongoni mwa sababu zilizoanishwa katika Ripoti Kuu ya Mwaka ya Ukaguzi wa Mashirika ya Umma kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ya Mkaguzi na mbidhibiti wa hesabu za serikali (CAG) imebaini kuwa deni linalohusu urejeshaji wa mikopo kutoka kwa wanufaika limeongezeka kutoka shilingi bilioni 123.04 hadi kufikia shilingi bilioni 931.14.

Ripoti hiyo pia inabainisha kuongezeka kwa utegemezi wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kutoka serikalini katika ukaguzi na tathmini ya vyanzo vya fedha kwa kipindi cha miaka mitano(2019/20 hadi 2023/24).

HESLB inategemea kwa kiwango kikubwa marejesho ya mikopo na fedha kutoka serikalini kama chanzo kikuu cha ufadhili wake. Utegemezi huo, umekua kwa asilimia 84 ndani ya miaka mitano kutoka Sh bilioni 255.62 mwaka 2019/20 hadi Sh bilioni 469.67 mwaka 2023/24.

Kwa upande mwingine, marejesho ya mikopo yalipungua kwa asilimia 7, kutoka Sh bilioni 190.72 mwaka 2019/20 hadi Sh bilioni 176.61 mwaka 2023/24 huku mahitaji yakiongezeka na urejeshaji wa mikopo kutokidhi viwango. Kwa mujibu wa Ripoti ya CAG, ucheleweshaji huo wa marejesho unatokana na ukosefu wa ufuatiliaji wa kutosha wa wadaiwa.

Hali hiyo inatokana na kutokuwa na mbinu za kutosheleza kukusanya mikopo na kuwekeza fedha kwani mifumo haina uwezo wa kufuatilia wahitimu wasio katika ajira rasmi. Ripoti inabainisha kuwa, endapo ufadhili wa serikali utapungua unaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa uwezo wa HESLB kutoa mikopo na kukidhi mahitaji ya wanafunzi.

CAG anapendekeza Bodi ianzishe na kutekeleza mikakati ya vyanzo mbadala vya fedha vitakavyosaidia uzalishaji wa fedha na kupunguza utegemezi wa bodi kwa serikali. Aidha, itengeneze na kutekeleza mikakati madhubuti ya kuongeza urejeshaji wa mikopo kama vile kuimarisha juhudi za ukusanyaji wa madeni na kuboresha motisha za urejeshaji wa mikopo.

UKIREJESHA MKOPO UNAMSAIDIA MWINGINE

Amina Mwampangala ni miongoni mwa wahitimu wanaolipa mikopo ya elimu ya juu. Anasema kama asingepata mkopo huo, angeshindwa kuendelea na chuo hivyo anajali na kuona umuhimu wa kurejesha ili wengine wapate mikopo.

“Nilienda chuo kuripoti kwa mara ya kwanza nikiwa na lengo la kujaribu kupata mkopo na wakati naenda nilikuwa nasikilizia kama majibu ya mkopo ambayo ndo njia pekee itakayoamua niendelee na chuo au nirudi nyumbani,” anasema.

Anaongeza: “Kwa bahati nzuri, nilipata majibu kuwa nimefanikiwa kupata mkopo ilikuwa ni asilimia 55 na hiyo ilikuwa awamu ya tatu kiasi hicho kilinisaidia kuendelea na chuo yaani ningekosa tu nisingesoma kwa sababu wazazi wangu hawana uwezo wa kunisomesha.”

Kwa mujibu wa Amina, kwa sasa ameajiriwa serikali hivyo ni fahari kwake kuendelea kurejesha mkopo kidogo kidogo. Anashukuru serikali kwa hatua yake kuongeza mikopo ya elimu ya juu kwa kuwa wengi wao wanatoka katika familia zisizo na uwezo.

Alfred Zakaria ambaye ni mnufaika aliyemaliza kulipa mkopo wake, anasema mkopo huo ulikuwa muhimu kumwezesha kusoma kutokana na wazazi wake kutokuwa na uwezo. “Baada ya kuhitimu mwaka 2013, nilikaa miaka nane bila kuwa na ajira rasmi lakini nilikuwa naingiza kipato hivyo sikujua namna ya kurudisha mkopo huo. Hata hivyo, nilianza kulipa mkopo huo mwaka 2022 baada ya kuajiriwa na nilimaliza baada ya miaka miwili.”

SABABU ZA KUSHINDWA KURUDISHA

Ukosefu wa ajira na kipato duni unatajwa kuwa sababu kubwa ya wanufaika wa mikopo kushindwa kurejesha kwa wakati huku wengi wao wakidai serikali iwapatie ajira.

“Changamoto ni elimu yetu haituandia kujiajiri hivyo kila mhitimu akimaliza anasubiri kupata ajira rasmi na kwa sababu hiyo wahitimu watabaki kulaumu serikali kwamba haitoi ajira, lakini hakuna asiyetaka kulipa ni hali ya maisha tu,” anasema mmoja wa wadau wa elimu.

Kwa mujibu wa Alfred, Bodi ya Mikopo inapaswa kuweka mfumo rahisi wa kidigiti utakaorahisisha ulipaji wa kiasi kidogo kidogo kwa njia ya simu ili wanufaika wa mikopo wasioajiriwa kwenye sekta rasmi warejeshe mikopo yao.

“Kuna ambao ni wafugaji, wakulima, wafanyabiashara, bodaboda hawa wote wanaingiza kipato na wanaweza kulipa hata kidogo kidogo hivyo, mifumo kama hiyo ni muhimu ili wadogo zetu na watoto wetu wasome,” anasisitiza.

Anasema miongoni mwa sababu za wanufaika kutorejesha mikopo pia ni kampeni duni ambazo haziwafikii wanufaika na jamii ili kutoa hamasa ya urejeshaji wa mikopo, hivyo anashauri kufanyika kwa kampeni za uelimishaji kuhusu umuhimu wa urudisha mikopo. “Vijana wengi wako mitandaoni hivyo watumie njia za kijigiti na akiliunde (AI)…. Ni vizuri mifumo ikasomana hata kwa mamlaka ya mapato,” anasema.

Akaongeza: “Kuna watu wana TIN (Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi) na wanaweza kuwatambua kwa namna hiyo na iwe lazima kwa anayetaka mkopo awe na TIN namba ili iwe rahisi kuwafatilia, lakini pia kuna namba za NIDA (Utambulisho wa Taifa zilizosaijiwa katika mifumo ya benki na simu, hivyo mnufaika anaweza kufuatiliwa kwa namna hiyo.” Anasema elimu kuhusu mikopo hiyo inapaswa kutolewa tangu wanufaika wanapokuwa vyuoni ili wawe na mwamko wa kurejesha mikopo kupitia mifumo rahisi ya kulipa.

WACHUMI,WADAU WATAKA MABADILIKO

Mtaalamu wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Godvictor Lyimo anasema utafiti unaonesha kuwa kuna utayari mdogo wa kurejesha mikopo ya elimu ya juu kwa sababu mikopo hiyo si ya dhamana. Anasisitiza kuchukuliwa hatua muhimu ikiwemo kutoa elimu kwa waliohitimu, kuwa na taarifa kanzidata zitakazoambatana na mfumo wa ufuatiliaji wa wadaiwa na kutambua hali zao za kipato.

“Napendekeza waanzishe mfumo wa ujumbe wa simu kuwakumbusha na kuwaelekeza namna ya kulipa mikopo kama ilivyo kwa benki na inawezekana wapo ambao hawako tayari kwa hao TIN na NIDA zitumike kuwapata, hivyo washirikiane na kampuni za simu na benki kupitia teknolojia kurahisisha ukusanyaji,” anasema.

Naye Mtaalamu wa Uchumi, Profesa Haji Semboja anasema mfumo wa ulipaji uliopo unapaswa kuangaliwa zaidi kwani wahitimu wengi hawapo kwenye mfumo rasmi. “Ufuatiliaji wa karibu unahitajika zaidi baada ya kumaliza vyuo na kuweka mifumo rahisi kwa hao vijana na kulipa mkopo iwe ni jambo la lazima kama mnufaika anaingiza kipato hata walipe kidogo kidogo,” anasema.

Kwa mujibu wa Profesa Semboja, Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu haina budi kujifunza katika nchi zilizofanikiwa ili  kujua namna bora ya kuhamasisha, kufuatilia na kukusanya mikopo. Mdau wa Elimu kutoka Taasisi ya Haki Elimu, Florige Lyelu anasema changamoto iliyopo ni kuwa, asilimia kubwa ya Watanzania ni wa kipato cha chini na pia, mwamko wa elimu kufundisha kujiajiri ni mdogo.

“Mimi nasisitiza waweke mfumo wa hiari kwa mnufaika yeyote atakayetaka kupunguza hivyo mfumo utengenezwa, lakini usiwe wa kuwabana sana lakini zaidi waunganishe mifumo yao na taasisi nyingine muhimu kama Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na BRELA inayosaijili wafanyabishara,” anasema Lyelu.

HESLB YAELEZA  MIKAKATI MIPYA

Mkurugenzi Mkuu wa HESLB, Dk Billy Kawia anasema wamepitia upya mifumo yao ikiwemo mifumo ya malipo inaorahisisha mnufaika kuingia na kurejesha mkopo. “Hata waajiri sasa tumewarahisishia kazi; zamani ilikuwa makaratasi, lakini  sasa waajiri wanaingiza taarifa za wanufaika kwenye mfumo na sisi tunaziona kama kuna upungufu tunawaambia,” anasema.

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, HESLB inachukua marejesho ya mkopo kwa wanufaika wote wenye kipato hata wakiwa katika ajira isiyo rasmi. “Kwa wale ambao hawapo katika mfumo rasmi, anaweza kulipa. Mwezi huu tumezindua rasmi kampeni ya ‘Kiduchu’ inayolenga kuwafuata wale ambao hawapo katika ajira rasmi kuanza kurejesha mkopo. Kwa hiyo, aliyeko mtaani labda anaendesha bodaboda, au mamalishe anaweza kulipia… Tuna mfumo unaitwa ‘Online Loan Repayment System’ akiingia atapata maelekezo,” anasema.

Anatoa wito kwa wanufaika wanaodaiwa kurejesha kwani sasa mifumo yao inasomana hivyo, watamfikia kila mtu ambaye ni mnufaika mwenye kipato. “Anaweza kulipa hata Sh 5,000 kidogo kidogo. Kwenye simu tupo kwa mfumo wa GPJ  na tuna  ‘app’ yetu inaitwa HESLB na mnufaika anaweza kulipa,” anasema.

Kwa mujibu wa Dk Kawia, kwa HESLB suala la utoaji elimu kuhusu urejeshaji ni muhimu na tayari wanafanya zoezi la kutoa semina nchi nzima kuhusu namna ya kurejesha mikopo “Wananchi wahudhurie hizi elimu na semina zetu ziko kila mahali. Hata mwaka huu, tumeshaanza huduma ndani ya jamii nchi nzima tunapoenda huko, tunaomba waje ili wapate elimu maana pia, mnufaika akiingia kwenye HESLB anakuta maelekezo,” anasema. Dk Kiwia anasema HESLB imeanzisha televisheni kupitia mitandao ya kijamii inayotumika kutoa elimu ili kila mtu sahihi apate elimu.

MAFANIKIO UKUSANYAJI MAPATO

Kwa mujibu wa Dk Kiwia, hadi sasa wamekusanya asilimia 70 ya mikopo iliyoiva ambapo kitakwimu wanaongoza barani Afika na Asia. Anasema tangu kuanzishwa kwa bodi wameshatoa Sh trilioni 9.5 kwa wanafunzi wanufaika milioni 1 na kwamba kwa wastani, katika kila nyumba kuna mtu mmoja aliyefikiwa na mkopo wa elimu.

Anasema mwaka mwaka 2022 HESLB ilikusanya Sh bilioni 169, mwaka 2023 ni Sh bilioni 177, mwaka 2024 ikakusanya SH bilioni 194.5 na mwaka 2025/2026 wamefikia zaidi ya Sh bilioni 220 huku akibainisha kuwa, serikali ilitoa Sh bilioni 916.7 kwa ajili ya mikopo ya elimu ya juu.

“Wakati Rais Samia anaingia madarakani tulikuwa tunapokea shilingi bilioni 560. Kwa mwaka huu tumepokea Sh bilioni 916.7 na mwaka unaoanza Julai mwaka huu, tutapata zaidi ya Shilingi trilioni 1,” anasema Dk Kiwia. Anaongeza: “Tumeendelea kuvunja rekodi ambayo haijawahi kutokea tangu bodi kuanzishwa kwa sababu wakati inaanzishwa, tulikuwa tunakusanya bilioni 50 sasa tunakusanya bilioni 240.”

Anakiri kuwa, changamoto kubwa ni hali ya uchumi kwa wanufaika kukosa ajira au kipato pamoja na ukosefu wa elimu ya namna ya kurejesha mikopo. “Tunajitahidi kutoa elimu sehemu mbalimbali kama kwa wafanyabiashara wadogo, mikutano ya wawekezaji, shuleni na hata katika vituo vya chumi,” anasema.

Anaongeza: “Sasa tunaenda mtandaoni kutengeneza maudhui katika mitandao ya kijamii ili kijana popote alipo saa 24 aone na kupata taarifa sahihi… Kwa kufanya hivyo, tunaamini tunaweza kufikia wanufaika wengi zaidi na wataweza kuresha mikopo.”

Anasema bodi imerahisisha mfumo wa kurudisha mikopo kwani sasa mnufaika anaweza kuanza kulipa kidogo kidogo kuanzia Sh 5,000 hivyo wanufaika wasiwe na woga wa kurudisha mikopo. “Tunakaribia kufungua dirisha letu la mikopo; wawe wanafuatilia matangazo yetu kwenye vyombo vya habari kuhakikisha wanapata  taarifa sahihi ,vijana kutumia fursa hii.

BODI YAJIPANGA KUONGEZA MAPATO

Dk Kiwia anasema bodi iko katika mpango wa ushirikiano na wadau wengine kuongeza ufadhili wa masomo badala ya kutegemea serikali pekee. “Mwaka jana tulipitisha sheria kwamba na sekta binafsi wachangie mpaka sasa kuna taasisi tatu zimejitokeza na kuna kampuni binafsi; tuko katika mazungumzo ili kuona namna ya kutusaidia vijana wasome,” anasema.

Hatahivyo, anatoa wito kwa taasisi zote kujitokeza kwa sababu lengo lao ni kumpa fursa kijana kupata elimu. SOMA : Kilichobainika ‘kupishana’ Wizara ya Elimu, Bodi ya Mikopo

 

Habari Zifananazo

One Comment

  1. When someone writes an piece of writing he/she retains the plan of a user in his/her mind that how
    a user can be aware of it. Therefore that’s why this post is perfect.
    Thanks!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button