Wananchi kunufaika na maduka jongefu ya Vodacom

DAR ES SALAAM: Wananchi katika maeneo yenye upatikanaji mdogo wa huduma za mawasiliano wanatarajiwa kunufaika zaidi baada ya Kampuni ya Vodacom kuzindua maduka jongefu sita yaliyoboreshwa, hatua iliyoongeza idadi ya maduka hayo kufikia 12 nchini.
Kupitia maduka hayo, wananchi watapata huduma mbalimbali karibu na maeneo yao ikiwemo usajili wa laini za simu, huduma za kifedha, huduma kwa wateja, ununuzi wa vifaa vya mawasiliano na simu janja kwa utaratibu wa malipo ya awamu pamoja na elimu ya matumizi ya teknolojia za kidijitali.
Hatua hiyo inatarajiwa kupunguza gharama na muda ambao wananchi walikuwa wakitumia kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hizo, huku ikichochea ujumuishwaji wa kifedha na matumizi ya teknolojia katika shughuli za kila siku.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Vodacom Philip Besiimire, alisema uwekezaji huo unalenga kupeleka huduma moja kwa moja kwa wananchi wanaozihitaji zaidi, hususan katika maeneo ya pembezoni.
Aidha, kila Duka Jongefu lina uwezo wa kuhudumia takribani wateja 1,200 kwa mwezi, jambo linalotarajiwa kuongeza upatikanaji wa huduma za mawasiliano na kidijitali kwa maelfu ya wananchi nchini.

Maduka hayo yatafanya kazi kwa mfumo wa mzunguko katika maeneo mbalimbali ya nchi ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanafikiwa na kunufaika na huduma hizo bila kulazimika kusafiri umbali mrefu.
Kwa ujumla, uwekezaji huo unatarajiwa kusaidia maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa kuongeza upatikanaji wa huduma za kidijitali, kuimarisha ujumuishwaji wa kifedha na kufungua fursa zaidi kwa wananchi na biashara katika maeneo mbalimbali ya Tanzania.



