Mwinyi kuwakilisha Tanzania mkutano wa bahari

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi, amewasili jijini Mombasa kwa ziara ya kikazi ya siku mbili ambapo atamwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan, katika Mkutano wa 11 wa Kimataifa wa Masuala ya Bahari unaofanyika nchini Kenya.

Rais Dk. Mwinyi aliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Moi, Mombasa, leo Juni 17, 2026, akiwa ameambatana na mkewe, Mama Mariam Mwinyi, pamoja na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Ngwaru Maghembe, na wajumbe wengine wa Serikali.

Mara baada ya kuwasili, Rais Dk. Mwinyi alipokelewa na Waziri wa Michezo, Uchumi Ubunifu na Vijana wa Kenya Salim Mvurya, Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi wa Zanzibar, Masoud Ali Mohamed, pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Bernard Yohana Kibesse.

Ziara hiyo inafanyika wakati mataifa mbalimbali duniani yakielekeza nguvu katika mijadala kuhusu uhifadhi wa bahari, matumizi endelevu ya rasilimali za baharini na kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi zinazoathiri mifumo ya ikolojia ya bahari.

Katika mkutano huo wa 11 wa Masuala ya Bahari (Our Ocean Conference), viongozi, wataalamu wa mazingira, wadau wa uchumi wa buluu na mashirika ya kimataifa wanatarajiwa kujadili mbinu mbalimbali za kuimarisha usimamizi wa bahari na fursa za kiuchumi zinazotokana na rasilimali za majini.

Ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo unatajwa kuwa muhimu kutokana na nafasi ya nchi katika uchumi wa buluu, hasa kwa kuzingatia mwambao wake mrefu katika Bahari ya Hindi na mchango wa sekta za uvuvi, utalii wa baharini na usafirishaji katika maendeleo ya uchumi wa taifa.SOMA: Mgahawa wa Kijapani unavyonogesha utalii Zanzibar

Kwa kumwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan, Rais Dk. Mwinyi anatarajiwa kuwasilisha msimamo wa Tanzania kuhusu usimamizi endelevu wa bahari, uhifadhi wa mazingira ya baharini na matumizi ya rasilimali za majini kwa maendeleo ya kizazi cha sasa na kijacho.

Mkutano huo unaendelea kupewa umuhimu mkubwa duniani kutokana na kuongezeka kwa changamoto zinazohusiana na uchafuzi wa bahari, uvuvi haramu, mabadiliko ya tabianchi na haja ya kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika kulinda rasilimali za bahari kwa manufaa ya dunia nzima.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button