Ruaha Milling yachochea uzalishaji wa alizeti nyanda za juu

IRINGA: Katika mazingira ambamo Tanzania inaendelea kukabiliwa na pengo kubwa kati ya mahitaji na uzalishaji wa mafuta ya kula, hususan mafuta ya alizeti, Ruaha Milling Company Limited imeanzisha mkakati wa moja kwa moja vijijini unaolenga kuinua kilimo cha alizeti.
Mkakati huo umejikita katika kuongeza upatikanaji wa malighafi viwandani na wakati huohuo kuchochea ukuaji wa uchumi wa wakulima na taifa.
Kwa mujibu wa takwimu za sekta ya kilimo nchini, Tanzania hutumia kati ya tani 600,000 na 800,000 za mafuta ya kula kwa mwaka, huku mafuta ya alizeti yakichangia zaidi ya asilimia 80 ya mahitaji hayo.
Hata hivyo, uzalishaji wa ndani haukidhi zaidi ya asilimia 40 na 50 ya mahitaji, hali inayolazimu nchi kuagiza mafuta kutoka nje, na hivyo kuongeza mzigo wa fedha za kigeni.

Katika muktadha huo, maeneo ya Nyanda za Juu Kusini, hususan Iringa, Njombe na Mbeya, yameendelea kuwa sehemu muhimu ya uzalishaji wa alizeti nchini, yakichangia zaidi ya asilimia 35 ya alizeti yote inayozalishwa Tanzania.
Akizungumza katika shamba darasa lililopo Kijiji cha Ikuka, wilayani Kilolo, Afisa Shamba Msaidizi wa Ruaha Milling Company Limited, Benjamin Mbilo, anasema kampuni imeamua kubadili mfumo wa kawaida wa viwanda kwa kuwekeza moja kwa moja kwenye kilimo cha wakulima.

Anasema lengo kuu ni kufidia pengo la upatikanaji wa malighafi ya alizeti kiwandani, ambalo limekuwa likiongezeka kutokana na mahitaji ya mafuta ya kula nchini kuongezeka.
“Tumeona wazi kuwa bila kuongeza uzalishaji shambani hatuwezi kuwa na viwanda imara. Ndiyo maana tumeamua kuingia moja kwa moja kwa wakulima,” anasema Mbilo.

Kwa mujibu wa takwimu, Mkoa wa Iringa una maeneo mengi yanayofaa kwa kilimo cha alizeti, yakiwemo ya Kilolo, Iringa Vijijini na Mufindi.
Wataalamu wa kilimo wanasema uwezo wa mkoa huo unaweza kuwa mkubwa endapo mbinu bora za kilimo, mbegu bora na matumizi ya pembejeo yataimarishwa kikamilifu.
Maeneo hayo yana uwezo mkubwa wa kuzalisha alizeti kutokana na kuwa na mvua za uhakika na ardhi yenye rutuba, ingawa changamoto ya upungufu wa mbolea na elimu ya kilimo imekuwa ikipunguza tija.

Mkakati wa mnyororo wa thamani: kutoka shamba hadi soko
Kupitia ushirikiano na Ruaha Milling na taasisi ya utafiti wa kilimo CIAT inayotekeleza mradi wa “Growing Together (Tukue kwa Pamoja)”, mkakati ni kuboresha mnyororo wa thamani wa alizeti.
Mkakati huo unahusisha uanzishwaji wa mashamba darasa zaidi, mafunzo ya kilimo bora, mikopo ya pembejeo (mbegu na mbolea), na ushirikiano na taasisi za kifedha.

Kwa mujibu wa wataalamu, mfumo huu unaweza kuongeza uzalishaji wa alizeti kwa wakulima wadogo kati ya asilimia 30 hadi 70, endapo utafuatwa kikamilifu.
Meneja Masoko wa Ruaha Milling Company Limited, Yasinta Kipeto, alitoa uchambuzi mpana kuhusu mabadiliko ya sekta ya kilimo na biashara ya mazao.
Anasema kampuni ilianza shughuli zake mwaka 1995, na baadaye kusajiliwa rasmi mwaka 2015, hatua iliyoiwezesha kufanya kazi kwa mfumo wa kibiashara zaidi na kupanua wigo wa ununuzi wa mazao.
Yasinta anasema kampuni inajikita katika mazao makuu matatu ambayo ni mpunga, mahindi na alizeti.
Mazao hayo yanatoka kwa wakulima wa Iringa, Njombe, Songea na Mbarali, maeneo ambayo kwa pamoja yanachangia sehemu kubwa ya chakula na malighafi za viwanda nchini.
Yasinta alieleza kuwa moja ya mageuzi makubwa waliyofanya ni kuwawezesha wakulima kuachana na ununuzi wa makadirio (madebe) na kutumia mfumo wa mizani.
“Kwa mfumo huu, mkulima tunamlipa kwa kilo halisi na hivyo uwazi wa biashara unaongezeka, upotevu wa haki unazuiwa na mkulima anaweza kupanga uzalishaji wake kwa hesabu,” anasema.
Anasema hatua hii imewasaidia wakulima kuelewa kuwa kilimo ni biashara yenye faida inayohitaji ufuatiliaji wa gharama na mapato.
Kwa mujibu wa Yasinta, sekta ya alizeti ina uwezo wa kuchangia asilimia kubwa ya mafuta ya kula yanayozalishwa nchini endapo uzalishaji utaongezeka.
Aidha, anasema ongezeko la uzalishaji wa alizeti linaweza kupunguza uagizaji wa mafuta kutoka nje, kuongeza ajira vijijini, kuimarisha viwanda vya ndani na kuongeza mapato ya kodi kwa serikali.
Hata hivyo anasema kiwanda chao cha kusindika alizeti ili kuzalisha mafuta ya kula kimeshindwa kufikia kiwango chake cha uzalishaji kutokana na ukosefu wa malighafi hiyo.
Anasema mahitaji yao ni gunia za alizeti kati ya 50 na 60 kwa siku sawa na gunia zaidi ya 15,000 kwa mwaka lakini hawapati kiasi hicho kwasababu ya uzalishaji mdogo mashambani.
“Ujumbe wetu mkubwa kwa wakulima ni kwamba kilimo cha alizeti hakipaswi kuendelea kuonekana kama utamaduni wa maisha ya vijijini bali kama biashara yenye tija,” amesema.
Kwa upande wake, Inoti Ibrahim kutoka CIAT anasema mradi wa “Growing Together” unalenga kumwezesha mkulima kuongeza uzalishaji kupitia mbinu bora za kisasa.
Anasema wakulima wanahamasishwa kupima udongo kabla ya kupanda, kutumia mbolea sahihi, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, na kutumia mbegu bora zenye tija.
Aliongeza kuwa matumizi ya mbolea za asili kama samadi ni muhimu katika kuhakikisha rutuba ya muda mrefu ya ardhi.
“Tuna amini haya yote yakizingatiwa, uzalishaji katika maeneo mnalimbali utongezeka kutoka chini ya gunia tano kwa heka moja hadi gunia 12 hadi 15.
Wakulima waliopata mafunzo wameeleza mabadiliko makubwa ya kiakili na kiuchumi baada ya kunufaika na juhudi za Ruaha Milling Company za kurejesha hadhi ya zao la alizeti na kulifanya zao la kibiashara.
Felix Lumso Msemwa anasema ana matumaini ya kuongeza uzalishaji kutokana na elimu mpya.
Nesia Msemwa anasema amebadilika kutoka kilimo cha mazoea kwenda kilimo cha kitaalamu na sasa anaona uwezekano wa kuongeza kipato.
Fausta Mnogawale anasema elimu hiyo imefungua macho yake na sasa anaona kilimo kama biashara halisi.
Mkulima kiongozi katika kijiji hicho cha Ikuka Angelo Kapene anasema wakulima wengi sasa wameanza kutumia mbegu bora na kuona alizeti kama zao la biashara.
Anasema mashamba darasa yamewasaidia kuona tofauti kubwa ya mavuno kati ya mbegu za kisasa na za kienyeji.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Ikuka, Salomoni Maginga, anasema zaidi ya wakazi 2,700 wa kijiji hicho wanategemea kilimo na wengi wao wameanza kuifanya alizeti kuwa moja ya mazao yao makuu badala ya kulichukulia kama zao la ziada.
Mtendaji wa kijiji, Riziki Mpogole, anasema kilimo ni nguzo ya uchumi na elimu kutoka Ruaha Milling imeongeza tija na uelewa wa soko.
Anasema mkakati wa Ruaha Milling Company Limited kwa kushirikiana na CIAT unaonyesha mwelekeo mpya wa kilimo cha alizeti katika kijiji chao—ambapo viwanda havisubiri malighafi, bali vinaingia moja kwa moja shambani.
Amesema kwa kuzingatia mahitaji ya kitaifa ya mafuta ya kula, nafasi ya alizeti inaendelea kuwa kubwa, na kama uzalishaji utaimarishwa, utegemezi wa mafuta ya nje utapungua na kuongeza mapato ya wakulima na taifa kwa kiwango kikubwa.



